IQNA

Waingereza laki moja watia saini ombi la kukamatwa Netanyahu

18:26 - September 05, 2015
Habari ID: 3358320
Harakati za makundi yanayowaunga mkono wananchi wa Palestina na kutetea haki za binadamu dhidi ya safari iliyopangwa kufanywa na Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni wa Israel na mazungumzo yake na viongozi wa Uingereza zimeshadidi na kushika kasi zaidi.

Kampeni ya Mshikamano na Wananchi wa Palestina ilitangaza jana kuwa tarehe 9 Septemba makundi yanayowaunga mkono wananchi wa Palestina na yanayopinga vita yatafanya maandamano mbele ya jengo la ofisi ya Waziri Mkuu wa Uingereza mjini London sambamba na kuwasili Waziri Mkuu wa Israel nchini humo. Taarifa ya muungano huo wa kiraia unaoundwa na makumi ya taasisi na jumuiya za kiraia zinazopinga vita na zinazowatetea wananchi wa Palestina imeashiria mashambulizi ya utawala wa kikatili wa Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza mwaka uliopita wa 2014 na kutangaza kuwa, Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu alihusika moja kwa moja na jinai za kivita zilizofanyika Gaza ambazo pia zimethibitishwa na Umoja wa Mataifa.
Wakati huo huo ombi la wananchi wa Uingereza la kutiwa mbaroni Netanyahu atakapowasili nchini humo, hadi sasa limesainiwa na raia karibu laki moja. Mtayarishaji wa ombi hilo katika mtandao wa intaneti, Damian Moran, anasema wananchi wa Uingereza hawataki kumkaribisha mtenda jinai za kivita. Ombi hilo linasema: Benjamin Netanyahu anakusudia kutembelea Uingereza, wakati sheria za kimataifa zinasema anapaswa kukamatwa na kutiwa mbaroni baada tu ya kuwasili nchini humo kwa makosa ya kutenda jinai za kivita na kufanya mauaji ya umati ya zaidi ya raia 2000 wa Palestina katika eneo la Ukanda wa Gaza hapo mwaka 2014.
Ombi hilo lililosainiwa na watu karibu laki moja linaashiria mauaji ya Wapalestina 2200 katika mashambulizi ya mwaka jana ya Israel dhidi ya watu wa Ukanda wa Gaza. Idadi kubwa ya wahanga hao walikuwa raia wa kawaida na watoto wadogo.
Wanaharakati wa kutetea haki za binadamu wanasema, iwapo saini za ombi hilo zitafikia laki moja basi itabidi liwasilishwe bungeni kwa ajili ya kuchunguzwa na kujadiliwa.
Kwa upande wake serikali ya Uingereza inadai kuwa safari ya Benjamin Netanyahu nchini humo ni safari rasmi na kwamba kwa mujibu wa sheria za kimataifa na zile za Uingereza, Netanyahu ana kinga ya kishtakiwa mahakamani.
Salem Allam ambaye ni mwanachama wa Kampeni ya Mshikamano na Palestina amekosoa baadhi ya vyombo vya habari vya Uingereza ikiwemo kanali ya BBC akisema vyombo hivyo vinanyamaza kimya mbele ya masaibu ya wananchi wa Palestina na siasa za ukandamizaji na mauaji za utawala wa Kizayuni wa Israel. Jumuiya mbalimbali za kimataifa pia ikiwemo ile ya Amnesty International, zimetoa ripoti zikiwatuhumu viongozi wa Israel kuwa wamefanya jinai dhidi ya wananchi wa Palestina. Hivi karibuni Amnesty International ilitangaza kuwa ushahidi unaonesha kwamba mauaji ya mamia ya raia wa Palestina yaliyofanywa na Israel katika Ukanda wa Gaza ni jinai ya kivita.
Wakati huo huo harakati za wananchi wa Uingereza na katika nchi nyingine nyingi za Ulaya za kususia bidhaa zinazozalishwa katika vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina zimepanuka zaidi katika miezi ya hivi karibuni. Kwa mfano tu jumuiya za kiraia za Uingereza hivi karibu zilifanya maandamano katika mji wa Birmingham na mbele ya kiwanda cha Elbit Systems. Kiwanda hicho na kampuni ya Rolls-Royce zinaipatia Israel injini za ndege zisizo na rubani (drones) ambazo hutumika kuua Wapaletina wasio na hatia yoyote.

3358037

captcha