IQNA

Zakir Naik, Mhubiri wa Kiwahhabi, apokonywa pasi na serikali ya India

22:10 - July 19, 2017
Habari ID: 3471075
TEHRAN (IQNA)-Zakir Naik, mhubiri wa Kiwahhabi mwenye utata amepokonywa pasi yake ya kusafiria na serikali ya India.

Taarifa zinasema serikali ya India imechukua uamuzi huo Jumanne baada ya serikali ya India kusema anatakiwa kujibu mashtaka kuhusu tuhuma za kufadhili ugaidi. Pasi ya kusafiria ya Naik, raia wa India, imechukuliwa na serikali ya nchi hiyo kufuatia ombi la Shirika la Kitaifa la Upelelezi (NIA)

Maafisa wa shirika hilo kuu la upelelezi India wanasema pasipoti hiyo imebatilishwa na Idara ya Kieneo ya Pasipoti ya Mumbai baada ya Naik kukataa kutii agizo la kufika katika idara za upelelezi kama alivyotakiwa kufanya mnamo Julai 13.

Naik alikuwa ametakiwa kufika katika idara hiyo ajitetee na aeleze kwa nini pasi yake haipaswi kubatilishwa kwa kuzingatia kesi kadaa dhidi yake.

Mhubiri huyo maarufu wa Kiwahhabi anakabiliwa na tuhuma za kufadhili ugaidi na pia utakasishaji fedha. Alitoroka India Julai 1, 2016 baada ya magaidi katika nchi jirani ya Bangladesh kudai kuwa walivutiwa na hotuba zake na wakaamua kutekeleza hujuma zao za kigaidi.

Vyombo vya habari India vinasema Naik tayari ameshapata uraia wa Saudi Arabia lakini hakuna chombo rasmi kilichothibitisha taarifa hiyo hadi sasa. Imedokezwa kuwa Mfalme Salman wa Saudia alimpa Pasi na hifadhi mhubiri huyo ili asikamatwe na Polisi ya Kimataifa, Interpol.

Tayari serikali ya India imeshapiga marufuku Taasisi ya Utafiti wa Kiislamu (IRF) inayosimamiwa na Dkt. Naik ambaye ana misimamo mikali na anayetambuliwa kuwa kiongozi wa Mawahhabi nchini India. Mhubiri huyo anamiliki pia televisheni iitwayo 'Peace TV' ambayo inahusika na uenezaji fikra za Uwahhabi. Wakuu wa India wanasema IRF ilipigwa marufuku kwa mujibu wa Kipengee cha 3 cha Harakati Zilizo Kinyume cha Sheria.

Mwezi Julai mwaka jana serikali ya nchi za Kiislamu ya Bangladesh iliipiga marufuku televisheni ya satalaiti ya 'Peace TV' inayofungamana na mhubiri Naik kwa tuhuma za kuunga mkono misimamo mikali na ugaidi na kuchochoea chuki za kidini na kimadhehebu. Serikali ya Bangladesh ilitoa amri ya kusitishwa matangazo ya televisheni ya satalaiti ya Peace TV yenye makao yake Dubai. Serikali ya Bangladesh imesema televisheni za nchini humo hazina idhini tena ya kurusha matangazo ya Peace TV kutokana na kuwa televisheni hiyo inaeneza misimamo mikali ya kidini na kuhimiza harakati za kigaidi kupitia mawaidha na hotuba ambazo hutolewa na Naik.

Tayari Zakir Naik ameshapigwa marufuku kuingia Uingereza na Canada na Peace TV imepigwa marufuku katika nchi ya Kiislamu ya Malaysia.

3620919

captcha