IQNA

Njama za Myanmar za kuwanyima chakula Waislamu ili watoroke nchi yao

21:32 - October 13, 2017
Habari ID: 3471214
TEHRAN (IQNA)-Shirika moja la kutetea haki za binadamu linasema serikali ya Myanmar inazuia kwa makusudi chakula kuwafikia Waislamu wa jamii ya Rohingya kwa lengo la kuwalazimisha kukimbia ardhi yao ya jadi nchini humo.

Kwa mujibu wa Tun Khin, mwenyekiti wa Jumuiya ya Burma nchini Uingereza, Waislamu wa jamii ya Rohingya sasa wananyimwa chakula ili wakimbie nchi. Amesema iwapo jamii ya kimataifa haitaishinikiza Myanmar hasa jeshi la nchi hiyo, basi kutashuhudiwa wimbi kubwa la Waislamu wataoikimbia nchi hiyo wiki zinazokuka. 

Akizungumza Ijumaa, Khin ametaka hatua za dharura zichukuliwe kuzuia masaibu zaidi kuwakumba Waislamu wa Rohingya wa jimbo la Rakhine la magharibi mwa nchi hiyo.

Siku ya Jumatano Ofisi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa ilikiri kuwa jeshi la Myanmar limetenda jinai dhidi ya Waislamu wa Rohingya.

Ofisi ya Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mjini Geneva imetangaza katika ripoti yake iliyoitoa jana kuwa vikosi vya usalama vya Myanmar vimewafukuza kinyama Waislamu nusu milioni wa jamii ya Rohingya katika jimbo la Rakhine na kuchoma moto nyumba zao, mazao yao ya kilimo na vijiji vyao kwa madhumuni ya kuwazuia Waislamu hao wasirudi tena katika eneo hilo.

Waislamu wa Rohingya wa Myanmar zaidi ya elfu sita wameshauawa na wengine elfu nane kujeruhiwa hadi sasa tangu tarehe 25 mwezi Agosti mwaka huu wakati lilipoanza wimbi jipya la mashambulizi ya ukandamizaji ya jeshi la nchi hiyo dhidi ya jamii hiyo ya walio wachache katika mkoa wa Rakhine.

3464150


captcha