IQNA

Inna Lillah wa Inna Ilayhi Rajioun

Kiongozi wa Tariqa ya Muridiyyah ya Senegal ameaga dunia

10:39 - January 11, 2018
Habari ID: 3471350
TEHRAN (IQNA)-Kiongozi wa Tariqa Muridiyyah (aṭ-Ṭariqat al-Muridiyyah) ya Senegal Sheikh (Serigne) Sidy Mokhtar Mbacke ameaga dunia akiwa na umri wa miaka 94.

Kwa mujibu wa mwandishi wa IQNA, mwanazuoni huyo ameaga dunia Jumanne usiku akiwa nyumbani kwake katika eneo la Niary Ngayme karibu na mji wa kidini wa Touba kati mwa Senegal.

Sheikh Sidy Mokhtar Mbacke alikuwa ni Khalifa wa Saba wa Tariqa ya Muridiyyah na alichukua nafasi hiyo Juni 30 mwaka 2010 baada ya kuaga dunia  Sheikh Mouhamadou Lamine Bara. Sheikh Mokhtar Mbacke alikuwa mjukuu wa kwanza wa mwanzilishi wa Tariqa hiyo, Sheikh Touba, kuchukua wadhifa wa ukhalifa na hafla yake ya mwisho ya umma ilikuwa Juni mwaka 2016 katika sherehe za Magal ambazo ni mjumuiko wa kila mwaka ya Tariqa ya Muridiyyah nchini Senegal. Kufuatia kuaga dunia mwanazuoni huyo, ambaye amezikwa katika maziara ya Makhalifa wa Taqriqa hiyo, Senegal imetangza maombolezo ya kitaifa.

Kufuatia kuaga dunia Sheikh Sidy Mokhtar Mbacke, siku ya Jumatano Tariqa ya Muridiyyah ilimteua Sheikh  Mountakha Mbacke kuwa kiongozi wake mpya.

Uteuzi huo umefuata taratibu za tariqa hiyo ambapo nafasi ya kiongozi mkuu anayeaga dunia huchukuliwa na mwanazuoni mwenye umri wa juu zaidi katika shajara ya ukoo huo.

Sheikh Mountakha Mbacke ni mwana wa Sheikh Mouhamadou Bassirou Mbacke Ibn Khadim Rassoul na ana umri wa miaka 88 huku akiwa anajishughulisha na ukulima mbali na harkati zake za kidini.

Aṭ-Ṭariqat al-Muridiyyah ya Senegal ilianzishwa na Sheikh Ahmadou Bamba  maarufu pia kama Aḥmad ibn Muḥammad ibn Ḥabīb Allāh, ambaye pia alikuwa na lakabu za Sheikh Touba na Khadim Rassoul na hivi sasa ni Tariqa yenye ushawishi mkubwa Senegal katika uga wa kidini, kisiasa na kiuchumi. Alizaliwa mwaka 1850 Miladia na kuaga dunia mwaka 1927 na alipata umashuhuri kwa kuongoza mapambano ya amani dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ufaransa. Makao makuu ya Tariqa hiyo ni katika mji wa Touba, ulioko kilomita 194 kutoka Dakar, mji mkuu Senegal.

Nchi ya Senegal iko katika pwani ya Afrika Magharibi na ilikoloniwa na Ufaransa kwa miaka kadhaa kabla ya kupata uhuru wake mwaka 1960 ambapo asilimia 92 ya watu wote milioni 15 nchini humo ni Waislamu. Tariqa nyingine yenye wafuasi wengi Senegal ni at-Ṭariqa al-Tijaniyyah.

3680984

captcha