IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mapambano ni njia pekee ya kukabiliana na utawala wa Kizayuni na kukomboa Palestina

10:09 - April 05, 2018
Habari ID: 3471454
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ametilia mkazo msimamo wa daima wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran wa kuiunga mkono kikamilifu Palestina na wapiga jihadi wake na kusema kuwa, tiba ya kadhia ya Palestina ni kuimarisha mrengo wa mapambano na muqawama katika Ulimwengu wa Kiislamu na kuzidisha mapambano dhidi ya utawala ghasibu wa Israel na waungaji mkono wake.

Ayatullah Sayyed Ali Khamenei ameyasema hayo Jumatano katika majibu yake kwa barua ya hivi karibuni ya Mkuu wa Idara ya Siasa ya Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina, Hamas, Ismail Hania. Amesema kuwa, harakati ya kuelekea upande wa kufanya mazungumzo na utawala laghai, mrongo wa ghasibu ni kosa kubwa lisilosameheka ambalo litachelewesha ushindi wa taifa la Palestina, na harakati hiyo haitakuwa na matokeo isipokuwa hasara kwa taifa hilo linalodhulumiwa.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema: Hapana shaka kwamba muqawama na mapambano ndio njia pekee ya kukomboa Palestina inayodhulumiwa na ndiyo dawa pekee ya kuponya majeraha ya mwili wa taifa hilo shujaa na lenye fahari.

Ameongeza kuwa: "Mambo yaliyosemwa katika barua ya Ismail Hania kuhusu changamoto kubwa za Umma wa Kiislamu, usaliti na unafiki wa baadhi ya nchi za Kiarabu na njama zao habithi za kumfuata Shetani Mkubwa yaani (Marekani) na vilevile jihadi ya Wapalestina ambao ni wanapambano wa mstari wa mbele katika kukabiliana na dhulma na jinai za adui, ni uhakika mtupu ambao sisi pia tunauunga mkono na tunaamini kwamba, ni wadhifa wetu kuwatetea na kuwaunga mkono kwa njia zote."

Ayatullah Khamenei amesema kuwa, hii leo njia pekee ya kurejea Umma wa Kiislamu katika izza na nguvu ni kusimama kidete mbele ya mabeberu na njama zao chafu na kwamba kadhia ya Palestina iko juu zaidi ya masuala yoye ya kimataifa ya Kiislamu.

Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema kuwa: Mataifa mbalimbali hususan vijana katika nchi za Kiislamu na Kiarabu na pia nchi zinazojitambua kuwa zinawajibika kuhusu kadhia ya Palestina zinapaswa kutekeleza kwa nguvu zote wadhifa huo mkubwa na kumlazimisha adui kurejea nyuma.

Itakumbukwa kuwa siku chache zilizopita Mkuu wa Idara ya Siasa ya Hamas, Ismail Hania alimwandikia barua Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu Ayatullah Ali Khamenei ambapo aliashiria njama kubwa zinazofanywa na mabeberu dhidi ya Quds tukufu na taifa la Palestina kwa shabaha ya kuiangamiza Ghaza ambayo ni ngome imara ya mapambano dhidi ya utawala wa Kizayuni wa Israel na hatimaye kukomesha kabisa mapambano dhidi ya utawala huo ghasibu na kurejeshwa uhusiano wa kawaida na watawala tegemezi wa nchi za Kiarabu. Ismail Hania pia alilishukuru taifa la Iran kutokana na misaada yake kwa Wapalestina na miongozo ya Kiongozi wa Mapinduzi ya Kiislamu kwa harakati ya Hamas.   

3703210

captcha