IQNA

Waislamu Hong Kong wazidi kuongezeka, wataka msikiti mpya

13:00 - April 15, 2018
Habari ID: 3471466
TEHRAN (IQNA)-Jamii ya Waislamu inazidi kuongezeka huko Hong Kongo, eneo lenye mamlaka ya kujitawala nchini China, na kwa msingi huyo kumeanzishwa jitihada za kujenga msikiti mpya ambao ujenzi wake umekwama kwa muongo moja sasa.

Katibu wa Muungano wa Waislamu wa Hong Kong Nadia Castro anasema hadi sasa wamekusanya US$ 38,200 kwa ajili ya ujenzi wa msikiti. Anasema michango inaanza kumiminika kila siku huku wakiwa na lengo la kukusanya US$ Milioni 1.27 katika kipindi cha mwaka moja. Mchango huo ni wa kujenga msikiti katika mji wa  Sheung Shui ulio katika jimbo la New Territories ambalo limeshuhudia ongezeko la kasi la Waislamu lakini la kusikitihsa ni kuwa hakuna msikiti.

“Kutokana na ongezeko la wahajiri Waislamu Hong Kong, kuna haja kubwa ya kuwa na misikiti na sehemu za Waislamu kujumuika pamoja kwa sababu za kidini na kijamii,” amesema Castro. Anasema hivi sasa wanaendesha shule kadhaa pamoja na vituo maalumu vya kuwahudumia wazee huku akibaini kuwa misitiki wanayojenga si sehemu ya kuswali tu bali inatumika pia kama kituo cha jamii.

Kuna Waislamu karibu  300,000 Hong Kong wengi wakiwa ni wahajiri kutoka Pakistan, Malaysia, India na Indonesia. Aidha kuna Waislamu 40,000 ambao ni Wachina wenyeji.

Kwa sasa kuna misikiti mitanoya kudumu Hong Kong huku kukiwa na msikiti moja wa muda na madrassah kadhaa. Kutokana na sehemu za kutohsa za ibada, Waislamu hulazimika kuswali katika vyumba maalumu au maeneo ya wazi.

Hong Kong ni eneo lenye utawala wa pekee ndani ya Jamhuri ya Watu wa China. Eneo hilo ilikuwa koloni la Uingereza kwenye pwani ya China kwa zaidi ya miaka 99, likarudishwa chini ya utawala wa Kichina mwaka 1997. Inaendelea kutawaliwa na sheria zake za pekee chini ya mamlaka kuu ya serikali ya Beijing.

 

3465542

 

captcha