IQNA

Mtoto mwenye umri wa miaka mitano amehifadhi Qurani kikamilifu Nigeria

18:35 - July 01, 2018
Habari ID: 3471579
TEHRAN (IQNA)- Mtoto mwenye umri wa miaka mitano nchini Nigeria amefanikiwa kuhifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu na hivi karibuni alishika nafasi ya pili katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani nchini Saudi Arabia.

Shamsudin Mohammad ni mwanafunzi katika Shule ya Kimataifa ya Professors mjini Zaria, katika jimbo la Kaduna kaskazini mashariki mwa Nigeria na imedokezwa kuwa alihifadhi Qur'ani kikamilifu akiwa na umri wa miaka mitatu na kwamba ameshawahi kushinda mashindano ya Qur'ani ya kijimbo na kitaifa. Shamsuddin Mohammad ambaye ni yatima alipoteza wazazi wake wawili akiwa na umri wa miezi sita na hivyo mustakabali ukawa hatarini wake akiwa bado mchango. Watoto wengi wenye hali yake na ambao wazazi wao hawakuwa na uwezo hujipata mitaani wakirandaranda kutafuta maisha kama ilivyo ada katika miji mikubwa ya kaskazini mashariki mwa Nigeria.

Lakini kwa bahati nzuri, baada ya wazazi Shamsudin Mohammad kufariki, Al Haj Shamsudin Aliyu alichukua jukumu la kumlea na akaamua kumsajili katika  Shule ya Kimataifa ya Professors akiwa na umria wa mwaka moja na nusu ili aweze kupata masomo ya kawaida na pia masomo ya Kiislamu. Akiwa hapo alifanya bidii na akawa miongoni mwa wanafunzi bora ambapo alihifadhi Qur'ani Tukufu kikamilifu baada ya miaka miwili. Alishiriki katika mashindano ya Qur'ani eneo hilo na akawa mshindi na kisha mwaka 2016 alishiriki katika mashindano ya kitaifa ya Qur'ani na akatangazwa mshindi. Mwaka 2017 alijiunga na washiriki kutoka nchi 50 katika mashindano ya kimataifa ya Qur'ani Saudi Arabia ambapo alishika nafasi ya pili.

Siku chachei zilizopita, katika kutambua kipawa chake cha Qur'ani na lugha ya Kiarabu,  Amiri wa eneo la Zazzau katika jimbo la Kaduna, Alhaji Shehu Idrisi, amemtunuku 'Nishani ya Ubora'.

Amiri wa Zazzau pia ameipongeza  Shule ya Kimataifa ya Professors kwa kuweza kuwalea watoto wenye uwezo mkubwa katika kuhifadhi Qur'ani Tukufu na pia katika nyanja za lugha yaKiarabu na taaluma zinginezo za sayansi na teknolojia.

3726534

captcha