IQNA

India yabadilisha jina la Kiislamu la mji wa Allahabad na kuupa jina la Kibaniani

21:17 - October 20, 2018
Habari ID: 3471714
TEHRAN (IQNA)- Watawala wa jimbo lenye idadi kubwa zaidi ya watu nchini India wamebadilisha jina la Kiislamu wa mji wa kihistoria ambao unajulikana kama Allahabad na kuupachika jina bandia la Kibaniani au Kihindu.

Allahabad ni mji wenye idadi ya watu zaidi ya milioni moja katika jimbo la Uttar Pradesh na sasa mji huo utapewa jina la Kibaniani la Prayagraj. Hayo yamedokezwa na afisa mwandamizi wa chama tawala cha Bharatiya Janata (BJP) ambacho wafuasi wake wana misimamo ya kufurutu ada ya Kihindu na aghalabu wana chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu.
Siddarth Nath Sing ambaye ni waziri wa afya katika jimbo la Uttar Pradesh amesema uamuzi huo ulichukuliwa katika kikao cha baraza la mawaziri kufuatia pendekezo la Waziri Kiongozi Yogi Adityanath ambaye ndiye msimamizi wa jimbo hilo.
Mji huo ni nyumbani kwa Waziri Mkuu wa kwanza wa India hayati Jawaharlal Nehru na uko kilomita 650 kusini mashariki mwa mji mkuu wa India, New Delhi. Mji huo ulipewa jina la Allahabad katika karne ya 16 wakati wa utawala wa Waislamu Wamughal.
Jina lake jipya, Prayagraj, linaashiria makutano ya mito ya Ganges na Yamuna, eneo ambalo hufanyika sherehe kubwa ya Kibaniani inayojulikana kama Kumbh Mela.
Chama cha BJP kimekuwa kikichukua hatua kadhaa za kuwakandamiza Waislamu nchini India tokea kiingia madarakani mwaka 2014.
Jamii ya wananchi wa India inaundwa na kaumu na dini mbalimbali na watu wa nchi hiyo wamekuwa wakiishi kwa amani na maelewano. Uhuru na mafanikio ya nchi hiyo yametokana na ushirikiano na mshikamano wa kitaifa wa India. Kwa msingi huo zinazochukuliwa na Wahindu wenye misimamo ya kuchupa mipaka dhidi ya Waislamu kwa kisingizio chochote kile yanaweza kuitumbukiza hatarini amani na umoja wa India.

3467012

captcha