IQNA

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu

Mwaka 1398 Hijriya Shamsiya ni mwaka wa "kustawi uzalishaji" Iran

9:52 - March 21, 2019
Habari ID: 3471884
TEHRAN (IQNA)- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, katika ujumbe kwa munasaba wa kuanza mwaka mpya wa 1398 Hijiria Shamsia, ametuma salamu za pongezi za Nowuruz (Nairuzi) na pia salamu kwa munasaba Wilada ya Imam Ali AS kwa wananchi wa Iran na hasa familia za mashahidi na majeruhi wa vita na amelitakia taifa la Iran mwaka wenye furaha, saada, afya ya kimwili na mafanikio ya kimaada na kimaanawi na ameutaja mwaka mpya kuwa mwaka wa "kustawi uzalishaji".

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei, katika tathmini yake kuhusu mwaka 1397 Hijria Shamsia uliopita, ameutaja kuwa mwaka  uliojaa pandashuka nyingi na kusema:  "Katika mwaka huo, adui alipanga njama nyingi dhidi ya Iran lakini taifa la Iran, liliweza kunawiri kwa maana halisi ya neno hilo na hivyo, kwa nguvu, muono wa mbali na hima ya vijana, njama hizo zimesambaratishwa."

Jibu la Iran kwa vikwazo vya Marekani na Ulaya

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesema taifa la Iran limetoa jibu imara na lenye nguvu kwa vikwazo shadidi vya Marekani na Ulaya katika nyuga za kisiasa na kiuchumi. Ameongeza kuwa: "Katika uga wa kisiasa, dhihirisho la wazi la jibu hilo ni maandamano makubwa ya 22 Bahman (11 Februari) na misimamo ya wananchi katika kipindi chote cha mwaka. Katika uuga wa makabiliano ya kiuchumi pia,  taifa la Iran limeweza "kuongeza ubunifu wa kisayansi na kiufundi", "kuimarisha kwa kiwango kikubwa mashirika ambayo msingi wake ni elimu", kuimarisha uundwaji wa miundo msingi ya ndani ya nchi kama vile kufunguliwa awamu kadhaa za vituo vikubwa vya uzalishaji gesi asilia kusini mwa nchi na kufunguliwa kituo kikubwa cha usafishaji mafuta cha Bandar Abbas."

Kiongozi Muadhamu amesema kwa hatua hizo za uga wa uchumi, taifa la Iran limweza kukabiliana na uhasama na ukhabithi wa maadui  na hivyo kuonyesha nguvu na adhama yake  na kwa msingi huo kuimarisha hadhi na heshima ya taifa, Mapinduzi na Mfumo wa Jamhuri ya Kiislamu.

Ayatullah Khamenei ameendelea kusema kuwa,  tatizo kuu la nchi linaendelea kuwa tatizo la kiuchumi na huku akiashiria kuongezeka matatizo ya kimaisha ya wananchi katika miezi ya hivi karibuni amesema: "Sehemu ya matatizo hayo inatokana na usimamizi usio sahihi katika uga wa masuala ya kiuchumi na hilo linapaswa kufidiwa." Amesema ingawa kuna mipango na tadbiri ya kukabiliana na matatizo hayo, tadbiri hiyo inapaswa kuzaa matunda katika mwaka mpya na wananchi wahisi taathira yake.

Wote wajitahidi kustawisha uzalishaji

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu ameashiria namna wananchi wa Iran waliovyoukaribisha mwaka uliopita wa 97 kwa kauli mbiu ya "Kuunga Mkono Bidhaa za Iran" , na athari chanya za kauli mbiu hiyo na kusema: "Mwaka huu, suala  la kimsingi ni " Uzalishaji" kwani iwapo uzalishaji utakuwepo, matatizo ya kimasiha na ajira yataweza kutatuliwa na pia nchi haitakuwa tegemezi kwa  maajinabi  na maadui na hata jambo hilo linaweza kwa kiwango kikubwa kutatua tatizo la thamani ya sarafu ya kitaifa. Kwa msingi huo naitangaza nara na kauli mbiu ya mwaka huu kuwa ni "Kustawi Uzalishaji".

Ayatullah Khamenei ametoa wito kwa wote kujitahidi katika kustawisha uzalishaji nchini na ameelezea matumaini yake kuwa, kwa kuimarika na kuboreka uzalishaji mwaka huu, matatizo ya kiuchumi yatachukua mkondo wa utatuzi.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu, ametuma salamu kwa roho toharifu ya Imam Khomieni MA na mashahidi watukufu, na salamu kwa Imam Waliul Asr- Mwenyezi Mungu Aharakishe Kudhihiri Kwake- na amemuomba Mwenyezi Mungu SWT alijaalie saada taifa la Iran na mataifa yote yanayoadhimisha Nowruz.

Siku Kuu ya Nowruz (Nairuzi)

Inafaa kuashiria hapa kuwa, leo ni tarehe Mosi Farvardin mwaka mpya wa 1398 Hijria Shamsia ambayo inasadifiana na siku ya kwanza ya mwaka wa Kiirani  yaani Sikukuu ya Nowruz au Nairuzi kwa wanaozungumza Kiswahili. Nowruz ni moja kati ya sherehe za kale zaidi duniani na ilianza kusherehekewa zaidi ya miaka 3000 iliyopita. Mbali na Iran nchi ambazo husherehekea Nowruz ni kama Afghanistan, Jamhuri ya Azerbaijan, Albania, Kyrgyzstan, Turkmenistan, Macedonia, India, Uturuki, Jamhuri ya Tatarstan nchini Russia, Sudan na Zanzibar nchini Tanzania. Mwaka 2010 Umoja wa Mataifa ulitangaza rasmi Machi 21 (yaani tarehe Mosi Farvardin) kuwa ni Siku ya Kimataifa ya Nowruz. Umoja wa Mataifa umeitambua Siku ya Nowruz kama siku kuu ya kale ambayo huadhimishwa wakati wa kuwadia msimu wa machipuo na kuhuishwa tena mazingira.

3799238/

captcha