IQNA

Qur'ani katika Mwezi wa Ramadhani

Ayatullah Khamenei: Usomaji wa Qur'ani ni sanaa takatifu

12:01 - March 13, 2024
Habari ID: 3478499
IQNA- Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amesisitiza kuwa, usomaji wa Qur'ani ni sanaa takatifu na inabidi lengo lake kuu liwe ni kuwafundisha watu na jamii maana na ujumbe uliomo kwenye Qur'ani na kuandaa mazingira ya kuzingatiwa aya za Kitabu hicho Kitakatifu kama ambavyo pia kilele cha istiqama ya wananchi wa Gaza kinatokana na kuielewa na kuifanyia kazi Qur'ani Tukufu.

Ayatullah Sayyid Ali Khamenei amesema hayo jijini Tehran usiku wa kuamkia leo Jumatano kwenye mahfali ya kushikamana na kuwa karibu na Qur'ani Tukufu ambayo yalifanyika jana usiku ambayo ilikuwa siku ya kwanza ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhani.

Aidha ameelezea kuridhishwa kwake na ongezeko la maqarii vijana wa Qur'ani Tukufu na kusema kuwa, ongezeko hilo ni katika neema kubwa za Mapinduzi ya Kiislamu.

Ameongeza kuwa, Qur'ani ni sanaa ya Mwenyezi Mungu na jukumu kubwa zaidi la qarii wa Qur'ani ni kufikisha maana na kuchora picha halisi ya Qur'ani katika maudhui tofauti ndani ya akili za wasikilizaji. Hivyo maqarii wa Qur'ani Tukufu ni mubalighina wa kweli wa risala ya Mwenyezi Mungu na wana wajibu wao wenyewe kabla ya jambo lolote kujipamba kwa sifa za mubalighina na wafikishaji wa risala ya Allah.

Kiongozi Muadhamu wa Mapinduzi ya Kiislamu amehimiza pia wajibu wa kuongezeka vikao vya Qur'ani Tukufu majumbani na Misikitini akisisitiza kuwa, kwenye vikao hivyo inabidi kuzingatiwe pia na kikamilifu suala la kufundisha maana na tafsiri za aya za Qur'ani Tukufu kwa ajili ya kupandisha juu kiwango cha maarifa ya kidini katika jamii.

Ayatullah Khamenei amegusia pia video iliyooneshwa kwenye kikao na majilisi hiyo ya Qur'ani ya jana usiku ikiwaonesha vijana wa Ukanda wa Ghaza huko Palestina wakisoma Qur'ani Tukufu wakiwa kwenye mazingira magumu sana na kusema kuwa, kilele cha istiqama na kusimama kidete tunachokiona leo kwa wananchi wa Ghaza kinatokana na kuielewa kwao Qur'ani Tukufu na kuifanyika kazi na bila ya shaka yoyote ushindi ni wa Wapalestina.

/3487545

Habari zinazohusiana
captcha