IQNA

Hamas: Kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni kunaupa kiburi cha kujenga vitongoji

13:45 - October 17, 2020
Habari ID: 3473268
TEHRAN (IQNA)- Harakati ya Mapambano ya Kiislamu ya Palestina (Hamas) imesema hatua ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala wa Kizayuni wa Israel imeupa utawala huo kiburi na ujuba wa kuendelea kupora ardhi za Wapalestina na kujenga vitongoji vya walowezi wa Kizayuni kinyume cha sheria.

Hazim Qassem msemaji wa Hamas amesema uamuzi wa utawala wa Kizayuni kujenga vitongoji vipya vya walowezi wa Kizayuni  katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan ni matokeo ya baadhi ya nchi za Kiarabu kuanzisha uhusiano na utawala huo ghasibu.

Wakati huo huo, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa mataifa matano ya barani Ulaya wametoa taarifa ya pamoja inayotaka kusitishwa mara moja ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kiyahudi katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mawaziri wqa Mashauri ya Kigeni wa Ufaransa, Uingereza, Ujerumani, Italia na Uhispania wamesema katika taarifa yao ya pamoja kwamba, wamesikitishwa na uamuzi wa viongozi wa Israel wa kujenga nyumba nyingine 4,900 katika maeneo yanayokaliwa kwa mabavu huko Palestina.

Ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu umeshika kasi zaidi tangu Rais Donald Trump aliposhika hatamu za uongozi nchini Marekani.   

Hayo yanajiri katika hali ambayo, hadi sasa hakujachukuliwa hatua yoyote ya kutekeleza azimio nambari 2234 la tarehe 23 Disemba 2016 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa linalotaka kusitishwa ujenzi wa vitongoji vya walowezi wa Kizayuni huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel. 

Umoja wa Falme za Kiarabu na Bahrain baada ya kufikia mapatano na utawala wa Kizayuni wa Israel unaoikalia Quds kwa mabavu; tarehe 15 mwezi Septemba mwaka huu zilisaini huko White mapatano ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala huo wa Kizayuni. Tukio hilo lilihudhuriwa na Rais Donald Trump wa Marekani na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.

3929658

captcha