IQNA

Asilimia 95 ya Wabahrain wanapinga uhusiano na utawala wa Israel

18:05 - October 18, 2020
Habari ID: 3473272
TEHRAN (IQNA) - Asilimia 95 ya wananchi wa Bahrain wanapinga hatua ya utawala wa kifalme nchini humo kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala haramu wa Israel.

Katika taarifa, Chama cha Kiislamu cha Al-Wefaq, ambacho ni chama kikubwa zaidi cha upinzani Bahrain kimetoa wito kwa Umoja wa Mataifa kuzuia wakuu wa Bahrain kuanzisha uhusiano na utawala wa Israel kwani waliowengi nchini humo hawajaafiki jambo hilo. Taarifa hiyo ya Al-Wefaq imekuja huku wanadiplomasia wa Israel na Marekani wakiwa wamefika katika mji mkuu wa Bahrain, Manama kwa ajili ya kutia saini taarifa ya pamoja kuhusu uanzishwaji rasmi uhusiano wa kidiplomasia baina ya Manama na Tel Aviv.

Tarehe 15 Septemba mwaka huu, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) na Bahrain walitia saini makubaliano ya kutangaza uhusiano wa kawaida baina ya nchi zao na utawala ghasibu wa Israel.

Sherehe hizo zilizofanyika katika Ikulu ya Marekani, White House, zilihudhuriwa pia na rais wa Marekani, Donald Trump na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala dhalimu wa Israel.

Chama cha Al-Wefaq kinasema wananchi wa Bahrain wanapaswa kupewa haki ya kubainisha maoni yao kuhusu mapatano hayo yaliyo kinyume cha sharia.

Tangu Februari mwaka 2011, wakati ulipoanza mwamko wa Kiisamu Asia Magharibi, Bahrain imekuwa uwanja wa maandamano ya amani ya wananchi wanaopinga utawala wa kifalme wa ukoo wa Aal Khalifa.
Wananchi hao wanataka kuwepo uhuru, utekelezwe uadilifu, ukomeshwe ubaguzi na kuundwa serikali itakayochaguliwa na wananchi wenyewe.
Hata hivyo kwa msaada wa wanajeshi wa Saudi Arabia na askari usalama wa Imarati waliotumwa nchini Bahrain kupitia mpango wa ulinzi wa Ngao ya Kisiwa, utawala wa Aal Khalifa unatumia mkono wa chuma kukabiliana na matakwa ya wananchi hao.
Kwa mujibu wa duru za haki za binadamu, Bahrain ina idadi kubwa zaidi ya wafungwa wa kisiasa kulinganisha na idadi ya watu katika nchi hiyo ndogo zaidi katika Ghuba ya Uajemi.

3929783

captcha