IQNA

Iran haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wake wa makombora ya kujihami

20:49 - October 19, 2020
Habari ID: 3473275
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Ulinzi wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesema nchi hii katu haitafanya mazungumzo kuhusu uwezo wa makombora yake ya kujihami.

Brigedia Jenerali Amir Hatami, ameyasema hayo Jumapili katika mahojiano na Kanali ya Habari ya Iran ambapo ameashiria kumalizika vikwazo vya silaha dhidi ya Iran na kusema imekuwa vigumu sana kwa Marekani kukubali kuwa Iran ina uwezo wa kujiundia silaha. Ameongeza kuwa, Marekani imekuwa ikiihadaa dunia kuwa hakuna nchi inayoweza kuwepo bila himaya ya Marekani.

Waziri wa Ulinzi wa Iran amesema vikwazo vya Marekani dhidi ya Iran vimekuwa chanzo cha nchi hii kustawi na kujitosheleza katika sekta ya ulinzi. Ameongeza kuwa: "Jamhuri ya Kiislamu ya Iran leo inaweza kuzalisha ndani ya nchi asilimia 90 ya mahitaji yake yote ya kijeshi.

Brigedia Jenerali Amir Hatami amesema katika kipindi cha mwaka mmoja uliopita Marekani imekuwa ikijaribu kufanya kila iwezalo kuhakikisha kuwa Iran haiondolewi vikwazo vya kuuza au kununua silaha zake lakini haikupata uungaji mkono kutoka kwa nchi yoyote katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Brigedia Jenerali Hatami ameashiria uwezo wa kijeshi wa Iran na kusema leo hata maadui wanakiri kwamba Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ni kati ya madola yenye nguvu kubwa za makombora duniani. Aidha amesema Iran pia ni kati ya nchi sita duniani zenye uwezo mkubwa katika uga wa kuunda ndege zisizo na rubani au drone.

Baada ya kumalizika muda wa vikwazo hivyo, sasa Iran iko huru kuuza na kununua silaha na zana za kivita nje ya nchi. Aidha vikwazo vya kusafiri nje maafisa 23 wa kisheria wa Iran vimeondolewa kwa mujibu wa azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa lililopasisha makubaliano ya JCPOA. 

Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran jana ilitoa tamko rasmi kufuatia kumalizika muda wa vikwazo vya silaha vya Iran na kusema:

Leo ni siku muhimu sana kwa jamii ya kimataifa ambapo kinyume kabisa na njama za utawala wa kibeberu wa Marekani, azimio nambari 2231 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na mapatano ya Mpango Kamili wa Pamoja wa Utekelezaji (JCPOA) vimeweza kulindwa.

3930209

captcha