IQNA

Mjumbe wa UN ana matumaini kuhusu mazungumzo ya amani ya Libya

14:39 - October 22, 2020
Habari ID: 3473286
TEHRAN (IQNA) - Kaimu mwakilishi wa Umoja wa Mataifa katika masuala ya Libya amesema kuwa, ana imani ya kufikiwa mkataba wa kudumu wa kusitisha mapigano nchini Libya kutokana na mazungumzo yanayoendelea kati ya pande hasimu.

Stephanie Williams, ameeleza kuwa, pande hizo tayari zimefikia makubaliano juu ya kufunguliwa tena kwa safari za anga na nchi kavu.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari mjini Geneva Uswisi, mwanadiplomasia huyo amesema pande hizo mbili, ambazo zinajadiliana huko Geneva wiki hii, pia zimekubaliana kudumisha "utulivu katika maeneo ya vita na kuepusha kuongezeka kwa mapigano".

Serikali ya Umoja wa Kitaifa, yenye makaazi yake mjini Tripoli, ambayo inatambuliwa na jamii ya kimataifa, na wapiganaji wa kundi la LNA) linaloongozwa na Marshal Khalifa Haftar, mbabe wa kivita mashariki mwa Libya, wanapigania udhibiti wa Libya kwa miaka kadhaa, kwa usaidizi wa nchi za kigeni.

Libya ilitumbukia katika machafuko na vita vya ndani baada ya wanajeshi wa Marekani wakishirikiana na wale wa Shirika la Kijeshi la Nchi za Magharibi (NATO) kuishambulia nchi hiyo na kusaidia harakati za kumuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa nchi hiyo  Muammar Gaddafi hapo mwaka 2011.

Tangu wakati huo, nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika imekuwa ikishuhudia vita vya ndani na machafuko ambayo yameharibu na kuvuruga kabisa maisha ya raia wa nchi hiyo na kutishia kutokea maafa ya kibinadamu.

3472897

captcha