IQNA

Stratijia ya Australia ya kuwa kitovu cha mfumo wa kifedha wa Kiislamu

12:01 - September 19, 2021
Habari ID: 3474313
TEHRAN (IQNA)- Australia ina mpango wa kuwa kitovu cha kieneo cha mfumo wa kifedha wa Kiislamu kutokana na kuwa ina uthabiti wa kisiasa, mfumo wa kifedha uliostawi na uchumi mkubwa wa ndani ya nchi.

Kwa mujibu wa taarifa ya tovuti ya eurekahedge, wengi hawajui kuwa Australia ilikuwa miongoni mwa nchi za kwanza duniani kuanzisha mfumo wa kifehda wa Kiislamu. Mashirika ya ushirika ambayo yanazingatia sheria za Kiislamu yamekuwa yakitoa huduma kwa watu binafsi na biashara ndogo ndogo nchini Australia tokea muongo wa 90. Tokea wakati huo sekta ya kifedha ya Kiislamu imekuwa ikistawi kwa kasi ya wastani lakini sasa kuna matarajio kuwa sekta hiyo itastawi kwa kasi kubwa katika miaka ijayo. Hivi sasa sekta ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu Australia imekuwa ikipania wigo wake kutoka huduma ndogo za ushirika na kuelekea katika hutoa huduma za kifedha kwa mashirika makubwa.

Australia ina idadi ndogo ya Waislamu lakini wengi ni matajiri na hivyo kuna haja ya kuwapa huduma za kifedha za Kiislamu. Kwa mujibu wa takwimu rasmi kuna Waislamu 475,000 kote Australia au asilimia 1.7 ya watu wote wa nchi hiyo. Pamoja na hayo uchunguzi uliofanywa na Bank of London and The Middle East (BLME) umebaini kuwa watu wa imani na tamaduni zote wanavutiwa na mfumo wa kifedha wa Kiislamu na hivyo hata wasiokuwa Waislamu wanatumia huduma za kifedha za Kiislamu nchini Australia.

Watu wengi wanavutiwa na maadili bora ya mfumo wa kifedha wa Kiislamu ambao unaharamisha riba na uwekezaji katika sekta haramu kama vile pombe,  kamari n.k.

3998278

captcha