IQNA

Mpango wa kujenga barabara kutoka Mashhad, Iran hadi Makka Saudi Arabia

21:49 - October 06, 2021
Habari ID: 3474391
TEHRAN (IQNA)- Kumetolewa pendekezo la kujengwa barabara kutoka mji mtakatifu wa Mashhad nchini Iran hadi mji mtakatifu wa Makka nchini Saudi Arabia.

Tovuti ya  arabicpost.net  imedokeza kuwa pendekezo hilo limetolewa na  Waziri Mkuu wa Iraq Moustafa Al Kadhimi katika mazungumzo yaliyofanyika hivi karibuni baina ya Iran na Saudia mjini Baghdad ambapo amesema kuwa barabara hiyo ipitie mji mtakatifu wa Karbala nchini Iraq kabla ya kufika katika mji mtakatifu wa Makka.  Duru za kidiplomasia zinadokeza kuwa katika kikao hicho cha mazungumzo baina ya Iran na Saudia, pande mbili zilifikia mpatano ya awali kuhusu baadhi ya masuala.

Mazungumzo hayo yalikuwa ya kwanza kufanyika baina ya Saudia na serikali mpya ya Rais Ibrahim Raiesi wa Iran. Mazungumzo baina ya Tehran na Riyadh yamekuwa yakiendelea kwa miezi kadhaa sasa kwa lengo la kurejesha uhusiano wa kawaida baina ya nchi mbili ambao ulivunjika mwaka 2016 baada ya Saudia kuchukua hatua ya upande mmoja kufunga ubalozi wake mjini Tehran.

Imearifiwa kuwa, Iran na Saudia zimeunga mkono pendekezo hilo la waziri mkuu wa Iraq la kujengwa barabara kutoka Mashhad hadi Makka.

Hayo yanajiri wakati ambao siku ya Jumatatu Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran alisema mazungumzo baina ya Jamhuri ya Kiislamu na Ufalme wa Saudi Arabia yanaendelea vizuri kwa lengo la kutatua matatizo yaliyopo baina ya pande mbili. Saeed Khatibzadeh, Msemaji wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Iran. Amebainisha kuwa, kumekuwepo na vikao kadhaa vya mazungumzo na serikali ya Saudi Arabia huko Baghdad nchini Iraq na kuongeza kuwa, kuna maendeleo ya kuridhisha katika mazungumzo yanayohusiana na usalama wa Ghuba ya Uajemi.

4002643

captcha