IQNA

OIC yalaani hatua ya Israel kubomoa maziara ya Wapalestina Quds

20:23 - October 13, 2021
Habari ID: 3474417
TEHRAN (IQNA)- Jumuiya ya Ushirikiano wa Nchi za Kiislamu (OIC) imelaani vikali kitendo cha utawala haramu wa Israel cha kubomoa maziara au makaburi ya Waislamu katika mji wa Quds, huko Palestina inayokaliwa kwa mabavu.

Katika taarifa, OIC imesema hatua ya mamlaka za utawala wa Kizayuni kubomoa na kufukua maziara ya Waislamu wa Palestina ya Mamilla na Al Yousifiah imeumiza nyoyo na kuchochea hisia za Wapalestina na Waislamu wote kwa ujumla.

OIC imesema kubomolewa makaburi hayo yenye zaidi ya miaka 1000 ni muendelezo wa utekelezaji wa sera za utawala haramu wa Israel, za kuhujumu matukufu na tamaduni za Kiislamu katika ardhi za Wapalestina zinazokaliwa kwa mabavu.

Hali kadhalika Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu imekosoa vikali hatua ya Rais wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA), Gianni Infantino kuhudhuria hafla ya ufunguzi wa kituo cha utamaduni cha Israel kilichojengwa katika moja ya sehemu palipobomolewa makaburi ya Palestina.

OIC imesema kitendo hicho kilichofanywa na Infantino Jumatatu iliyopita si tu kimeenda kinyume na thamani muhimu za michezo na kanuni za FIFA, lakini pia kimeonesha namna mkuu huyo wa FIFA anavyounga mkono ukaliaji wa mabavu wa ardhi za Wapalestina unaofanywa na utawala ghasibu wa Israel.

Jumuiya hiyo imesisitiza kuwa, kitendo hicho cha Rais wa Shirikisho la Kimataifa la Soka hakikubaliki na kinapaswa kulaaniwa kwa nguvu zote.

3476026

captcha