IQNA

Maandamano Bangladesh kulaani kuvunjiwa heshima Qur'ani katika hekalu la Wahindu

19:21 - October 14, 2021
Habari ID: 3474423
TEHRAN (IQNA)- Watu wasiopungua watatu wameuawa huku wengine kadhaa wakijeruhiwa katika maandamano ya kulaani kitendo cha kuvunjiwa heshima Qur'ani Tukufu nchini Bangladesh.

Kwa mujibu wa shirika la habari la Anadolu, maandamano hayo yalifanyika usiku wa kuamkia leo katika wilaya ya Chandpur, eneo la Hajiganj, kusini mashariki mwa mji mkuu Dhaka, ambapo maafisa kadhaa wa polisi ni miongoni mwa majeruhi.

Inaarifiwa kuwa, Waislamu waliokuwa na ghadhabu waliingia mabarabarani baada ya kupata habari ya kudhalilishwa na kuchafuliwa kitabu chao kitukufu katika Hekalu la Wahindu wilayani Comilla jijini Dhaka mapema jana Jumatano.

Duru za hospitali katika wilaya ya Chandpur zinaarifu kuwa, raia 10 na maafisa usalama 19 wamelazwa katika Hospitali ya Hajiganj baada ya kujeruhiwa kwenye maandamano hayo.

Maandamano mengine ya kulaani uafriti huo wa kukivunjia heshima kitabu kitukufu cha Waislamu nchini Bangladesh yamefanyika katika wilaya za Comilla, Chattogram, Kurigram, na Moulvibazar. Hali ya taharuki ingali imetanda katika maeneo hayo.

Waislamu wa Bangladesh wamekuwa wakijitokeza kwa wingi kushiriki maandamano ya aina hii. Oktoba mwaka jana, waliandamana kwa wingi kulaani hatua ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa ya kuunga mkono kitendo cha kifidhuli cha jarida la Kifaransa la Charlie Hebdo cha kuchapisha tena vibonzo vya kumvunjia heshima Mtume Muhammad SAW.

2391992

captcha