IQNA

Ibada ya Hija

Wamorocco wengi walazimishwa kughairi safari ya Hija kutokana na kupanda gharama

16:16 - June 13, 2022
Habari ID: 3475373
TEHRAN (IQNA) –Sawa na idadi kubwa ya Waislamu katika nchi nyingine, raia wengi wa Morocco wanalazimika kufuta safari yao ya Hijja mwaka huu kutokana na gharama kubwa.

Kulingana na wizara ya Masuala ya Kiislamu ya Morocco, wale waliochaguliwa Kuhiji mwaka wa 2022 watalazimika kulipa MAD 63,000 ($6,405), 27% zaidi ya gharama za mwaka wa 2019.

Wale wanaosafiri na mashirika ya usafiri ya kibinafsi watalazimika kulipa zaidi, kwani gharama za Hajj zitakuwa kati ya dirham 70,000 na 160,000 kulingana na hoteli, mkurugenzi wa wakala wa Travel 4 You, Houda al-Majdouli, amesema.

Waislamu kutoka sehemu mbalimbali za dunia humiminika Makka kila mwaka kutekeleza ibada ya Hija, mojawapo ya nguzo za Uislamu.

Kila Mwislamu mtu mzima mwenye uwezo na anayeweza kumudu kifedha safari hiyo lazima ahiji angalau mara moja katika maisha.

Serikali ya Saudi iliwawekea vikwazo mahujaji wa kigeni wa Hijja kwa miaka miwili kutokana na janga la COVID-19, ikiruhusu wageni 1,000 wa ndani mnamo 2020 na 60,000 mnamo 2021.

Ongezeko la gharama

Tatizo la gharama haliko Morocco pekee kwani Waislamu kutoka nchi nyingine pia wanabeba mzigo mkubwa.

Kwa mfano ikilinganishwa na nchi jirani, India, Pakistani, Indonesia na Malaysia, gharama ya kutekeleza Hija nchini Bangladesh ni ya juu kiasi.

Mahujaji wa Bangladesh watalazimika kulipa kima cha chini cha $5,332 kila moja mwaka huu, ambayo ni 47% zaidi ya gharama kwa mahujaji nchini Pakistan, na 93% zaidi, ikilinganishwa na hali ya Indonesia.

Waislamu wa Sri Lanka nao pia wametangaza mwaka huu hawataweza kutekeleza ibada ya Hija kutokana na ongezeko la gharama pamoja na matatizo makubwa ya kiuchumi katika nchi yao ambayo yamepelekea kuwepo uhaba mkubwa wa sarafu za kigeni.

Hivi karibuni pia, Mkuu wa Shirika la Hija na Ziyara za Kidini la Iran alisema maafisa wa Saudi bado hawajajibu malalamiko ya nchi kadhaa juu ya kuongezeka kwa gharama za Hija mwaka huu wa 1443 Hijria Qamaria sawa na 2022 Miladia.

Seyed Sadeq Hosseini alisema kuwa mazungumzo yamefanyika ili kupata punguzo kutoka kwa makampuni ya Saudia mwaka huu.

Huku akiashiria kupanda kwa bei, Hosseini ameongeza kuwa barua zimetumwa kwa Wizara ya Hija ya Saudi Arabia kuhusiana na suala hilo na kwamba nchi nyingine pia zimetoa malalamiko na wasiwasi wao lakini hakuna jibu rasmi la maafisa wa Saudi Arabia hadi sasa.

Mbali na kuongezeka kwa gharama za huduma, bei za bidhaa pia zimeongezeka, alisema, akibainisha kuwa kwa mfano, bei ya vyakula vya protini imeongezeka kwa asilimia 20 hadi 40.

Janga la COVID-19 imetajwa kuwa sababu kuu ya gharama za ziada za kusafiri kwa Hajj mwaka huu.

Gharama ya safari za ndege pia imepanda katika miaka ya hivi karibuni. Halikadhalika mfumuko wa bei nchini Saudi Arabia ni sababu nyingine iliyochangia kupande gharama za Hija.

Bei ya bidhaa na huduma nyingi katika Ufalme wa Saudia imepanda, kumaanisha kwamba gharama ya jumla ya safari pia imepanda.

3479284

captcha