IQNA

Hali nchini Tunisia

Sababu za Rais wa Tunisia kutaka Uislamu ufutwe kama dini rasmi nchini

23:18 - June 25, 2022
Habari ID: 3475425
TEHRAN (IQNA)- Rais wa Tunisia, Kais Saied alitangaza Jumanne (tarehe 21 Juni) kwamba Uislamu hautakuwa tena dini ya serikali katika katiba mpya, ambayo itapigiwa kura ya maoni Julai 25, na kwamba jina la Uislamu halitakuwemo tena katika katiba mpya ya nchi hiyo.

Kais Saied aliongeza kuwa: "Katika katiba mpya, hatuzungumzii serikali ambayo dini yake ni Uislamu, bali tunazungumzia taifa ambalo dini yake ni Uislamu. Umma unatofautiana na Serikali." Kuhusu utambulisho wa serikali katika katiba mpya ya nchi, Rais wa Runisia amesema: "Jambo muhimu si suala la serikali ya mfumo wa Rais au Bunge, bali muhimu kuliko yote ni kwamba mamlaka ya taifa."

Hapo awali, Tume ya Taifa ya Ushauri kwa ajili ya kutayarisha katiba mpya ya Tunisia ilipasisha kuondolewa kwa Uislamu kama dini rasmi ya nchi hiyo. Sadeq Belaid, mratibu wa Kamati ya Taifa ya Ushauri kwa ajili ya katiba mpya nchini Tunisia amesema: “Rais, kwa mujibu wa katiba mpya, atachagua waziri mkuu, na serikali itakuwa chombo cha kuwasilisha mipango na ubunifu, na kazi yake haitakuwa ya kiutendaji.” Hata hivyo, sura ya kwanza ya katiba ya Tunisia iliyoandikwa mwaka wa 2014, inasisitiza kuwa Tunisia ni "nchi huru, inayojitawala na yenye mamlaka, na kwamba Uislamu ndio dini ya nchi hii, lugha yake ni Kiarabu, na mfumo wake ni wa Jamhuri." 

Dhamira halisi ya Rais Saied

Hatua ya Rais wa Tunsia ya kuidhinisha kufutwa Uislamu kama dini rasmi ya nchi hiyo inaonyesha dhamira halisi ya Kais Saied, ambaye alichukua madaraka kwa njia inayoshabiana na mapinduzi kwenye nchi hiyo ndogo ya Afrika Kaskazini mnamo Julai 25, 2021. Katika hatua ambayo haikutarajiwa wakati huo, Kais Saied alisimamisha Bunge na kumfuta kazi spika wake, pamoja na waziri mkuu wa serikali, na kuchukua udhibiti wa mambo yote ya nchi. 

Kisingizio kilichotumiwa na Kais Saied kuhalalisha hatua hiyo ni madai kwamba, waziri mkuu na serikali wameshindwa kuboresha hali ya uchumi na kukabiliana ipasavyo na wimbi la maakimbuzi ya corona. Hatua hiyo ilizusha mvutano mkubwa wa kisiasa nchini Tunisia na tunaweza kuutaja kuwa ndio mgogoro mkubwa zaidi wa kisiasa wa nchi hiyo tangu baada ya vuguvugu la wananchi la mwaka 2011. Kais Saied pia amebadilisha wananchama wa Kamisheni Huru ya Uchaguzi na kutangaza kuwa katiba mpya itapigiwa kura ya maoni mwishoni mwa mwezi Julai mwaka huu.

Vyama vya kisiasa nchini Tunisa vimekuwa na misimamo tofauti kuhusiana na hatua hizo za rais wa nchi. Baadhi ya vyama hivyo vimeyataja maamuzi na hatua zake kuwa ni mapinduzi dhidi ya katiba ya nchi, huku vyama vingine vikisema kuwa hatua hizo ni kusahihisha mwenendo wa mapinduzi ya wananchi ya mwaka 2011. Wakati huo huo Kais Saied mwenyewe anadai kuwa, hatua hizo zimechukuliwa kwa mujibu wa katiba na kwa ajili ya kulinda nchi mbele ya hatari zinazoinyemelea.

Kufutilia mbali ushawishi wa Ennahdha

Hata hivyo ukweli ni kuwa, kiongozi huyo anakusudia kuwafutilia mbali wapinzani wake wakuu wa kisiasa, na kwa kutilia maanani ushawishi mkubwa wa chama cha Ennahdha katika siasa za Tunisia, Kais Saied anafanya kila awezalo kufuta jila la Uislamu katika katiba ya nchi hiyo na hivyo kupunguza satwa na ushawishi wa chama hicho cha Kiislamu baina ya wananchi wa Tunisia. Vilevile anatumia vyombo vya mahakama kuhakikisha kwamba, kiongozi wa chama hicho chenye mielekeo ya Kiislamu, Rached Ghannouchi anahukumiwa na kuswekwa jela.

Hatua hizi zimekabiliwa na upinzani mkubwa, hususan wa majaji wa Tunisia ambao wamekuwa wakimkosoa mara kwa mara kiongozi huyo kwa kuingilia na kuwawekea mashinikizo majaji. Kais Saied amewafukuza kazi majaji wanaokitetea chama cha Ennahda na hivyo amefungua njia ya kuwaandama na kuwafunguliwa mashtaka wapinzani wake wakuu, kama vile kiongozi wa Ennahda, Rached Ghannouchi, aliyekuwa spika wa bunge la nchi hiyo. Kabla ya kuvunjwa bunge, chama cha Ennahdha kilikuwa na mamlaka na nguvu kubwa zaidi katika taasisi hiyo ya kutunga sheria.

Kwa ujumla inatupasa kusema kuwa, hatua za Kais Saied katika kipindi cha mwaka mzima uliopita zimelenga kuhodhi madaraka ya nchi na kuwafutilia mbali wapinzani wake wakuu wa kisiasa.   

4065808

captcha