IQNA

Mapinduzi ya Kijeshi

Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu yalaani mapinduzi ya kijeshi Burkina Faso

20:40 - October 02, 2022
Habari ID: 3475869
TEHRAN (IQNA) – Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC) imelaani kuondolewa madarakani kwa rais wa Burkina Faso, Paul-Henri Damiba na maafisa wa kijeshi.

Katika taarifa yake siku ya Jumamosi, OIC ilisema mabadiliko hayo kwa nguvu yamekuja wakati jumuiya ya kimataifa imejitolea kuunga mkono Burkina Faso kuongoza mageuzi ya kisiasa ya amani ambayo yanaruhusu kufanyika kwa uchaguzi huru nchini humo.

Katibu Mkuu wa OIC Hissein Brahim Taha ametoa wito wa utulivu na kudumisha moyo wa mazungumzo na uwajibikaji ili kufikia matarajio ya wananchi wa Burkina Faso katika usalama na utulivu.

Ijumaa jioni, kundi la maafisa wa kijeshi wakiongozwa na Kapteni wa jeshi Ibrahim Traore walimwondoa Damiba, kuvunja serikali ya mpito na kusimamisha katiba.

Unyakuzi huo katika jimbo hilo la Afrika Magharibi ulikuwa wa pili katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja, ambapo Damiba mwenyewe alichukua mamlaka baada ya kumpindua aliyekuwa Rais wa nchi hiyo Roch Kabore mwezi Januari.

Wakati huo huo, Umoja wa Afrika (AU) umelaani hatua ya 'wanajeshi waasi' kutwaa mamlaka ya nchi kinyume cha katiba huko Burkina Faso, katika hali ambayo nchi hiyo ilikuwa katika mkondo wa kurejesha utawala wa kiraia.

Moussa Faki Mahamat, Mwenyekiti wa Kamisheni ya AU amesema katika taarifa kuwa, anatiwa wasiwasi na kurejea kwa wimbi la mapinduzi ya kijeshi katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, na mataifa mengine ya bara hilo.

Taarifa ya AU imesema: Mwenyekiti (wa Kamisheni ya AU) anatoa mwito kwa jeshi (la Burkina Faso) kujiepusha mara moja na hatua za ghasia au zinazoweza kutishia usalama wa raia, uhuru wa kiraia na haki za binadamu.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika ametoa mwito wa kurejeshwa utawala wa kikatiba nchini Burkina Faso kufikia Julai mwaka 2024 kama ilivyokuwa imeratibiwa kwenye mpango wa amani wa nchi hiyo.

Kabla ya hapo, Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Magharibi mwa Afrika (ECOWAS) ilieleza bayana kuwa, hatua ya wanajeshi hao kumuondoa madarakani mtawala wa kijeshi Paul-Henri Damiba ni kinyume cha katiba ya nchi hiyo.

3480698

captcha