IQNA

Umuhimu wa kushiriki katika Majlisi za Maombolezo Muharram + Video

TEHRAN (IQNA)- Imesisitizwa sana kuandaa na kushiriki katika Majlisi za kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika mwezi wa Muharram.

Akizungumza katika mfululizo hotuba fupi kuhusu Ashura, Dkt. Muhsin Ismaili amefafanua kuhusu mitazamo mbali mbali ya tukio la Ashura. Katika kikao chake cha nne amefafanua kwa muhtasari kuhusu umuhimu wa kuandaa na kushiriki katika Majlisi za kukumbuka kuuawa shahidi Imam Hussein AS.

Amesema kwa kushiriki katika vikao hivyo, tunaangazwa tena historia ya Ashura ili tusisahau tukio hilo muhimu na pia majlisi hizo hutuwezesha kutafakari na kupata mafunzi na ibra kwa ajili ya mustakabali wetu.

Katika mwezi wa Muharram Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, na wapenda haki kote duniani hukumbuka  tukio la Ashura ambalo lilijiri takribani miaka 1382 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria.

Katika tukio hilo, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

Wimbi la mwamako wa Imam Hussein AS dhidi ya madhalimu lilikuwa na taathira hiyo ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba haikuishia kwenye wakati, zama au eneo makhsusi bali imeendelea kufanyakazi yake kati ya wanadamu wote hadi katika zama hizi. Ukweli huu umethibitisha msemo unaosema: "Kila siku ni Ashura na kila ardhi ni Karbala."

3475482