IQNA

Kumuomboleza Imam Hussein AS ni kujenga mustakabali + video

19:44 - August 16, 2021
Habari ID: 3474194
TEHRAN (IQNA) – Kwa kumuomboleza Imam Hussein AS haungazii tu yaliyopita bali pia ni kuangazia na kujenga mustakabali.

Akizungumza katika mmfululizo wa mihadhara yake kuhusu ‘Somo la Ashura’, Dkt Muhsin Ismaili amefafanua kuhusu mitazamo mbali mbali ya ‘Tukio la Ashura’.

Katika somo lake la sita amezungumza kuhusu namna ambavyo maombolezo ya mwezi wa Muharram hujenga mustakabali.

Amesema hii ndio sababu katika Ziyara tunayosoma  siku ya Ashura huwa tunamuomba Mwenyezi Mungu atupe maarifa sawa na ya Imam Hussein AS na tuweze kuwa na istikama kama aliyokuwa nayo.

Amesema kuna hadhithi nyingi zinazoashiria kuwa kulia au kutoa machozi katika maombolezo ya Imam Hussein AS huwa na thawabu chungu nzima lakini  mbali na hisia hiyo maombolezo muhimu zaidi ni kuwa na maarifa sawa na ya mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW.

Katika mwezi wa Muharram Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, na wapenda haki kote duniani hukumbuka  tukio la Ashura ambalo lilijiri takribani miaka 1382 iliyopita kulingana na kalenda ya Hijria Qamaria.

Katika tukio hilo, moja kati ya vita mashuhuri katika historia ya Kiislamu na ya mwanadamu, vilitokea baina ya majeshi ya haki na batili katika ardhi ya Karbala huko Iraq. Siku hii inajulikana kwa jina la Ashura. Katika siku hiyo mjukuu wa Mtume SAW, Imam Hussein bin Ali bin Abi Twalib AS, alisimama kishujaa na wafuasi wake waaminifu 72, kukabiliana na jeshi la batili ili kuilinda dini ya Allah. Hamasa ya Karbala ilikuwa dhihirisho la mambo mawili makuu. Kwanza ni ujasiri, ushujaa, moyo wa kujitolea, uaminifu pamoja na kuyapokea kwa moyo mkunjufu mauti ya kuuawa shahidi, sifa walizojipamba nazo wapiganaji wachache wa jeshi la haki wakiongozwa na Imam Hussein AS dhidi ya Yazid bin Muawiya.

Wimbi la mwamako wa Imam Hussein AS dhidi ya madhalimu lilikuwa na taathira hiyo ilikuwa kubwa mno kiasi kwamba haikuishia kwenye wakati, zama au eneo makhsusi bali imeendelea kufanyakazi yake kati ya wanadamu wote hadi katika zama hizi. Ukweli huu umethibitisha msemo unaosema: "Kila siku ni Ashura na kila ardhi ni Karbala."

3475497

Kishikizo: imam hussein as ashura
captcha