IQNA

Muharram 1435

Waislamu katika miji ya Uganda, Tanzania na Kenya washiriki katika maombolezo ya Siku ya Ashura

11:51 - July 30, 2023
Habari ID: 3477357
NAIROBI (IQNA)- Waislamu, hasa wa madhehebu ya Shia, wamejumuika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi kuadhimisha kumbukumbu ya kuuawa shahidi Imam Hussein (as) katika siku ya Ashura.

Waislamu hao walimiminika katika mtaa mmoja katika matembezi (Masira) kwa mnasaba  kumbukumbu ya Ashura walisika wakipiga nara za Labbayka ya Hussein na kuonyesha mapenzi yao makubwa kwa Mjukuu wa Mtume Muhammad (SAW),  Imamu Hussein (AS). Matembezi kama hayo yameshuhudiwa pia katika miji mingine ya Kenya kama vile Mombasa, Nakuru na Lamu.

Maandamano hayo ya kumbukumbu ya Ashura nchini Kenya, ambayo yamefanyika Jumamosi, kwa mara nyingine tena yanathibitisha kuwa na nafasi muhimu miongoni mwa Wakenya mafundisho ya Ahlul-Bayt, sira na harakati ya Imamu Hussein (AS) iliyokuwa na lengo la kupinga dhulma na kutetea Uislamu.

Wakati huo huo katika nchi ya jirani ya Tanzania pia, mikoa mbalimbali ikiwemo ya Arusha, Singida, Tanga, Dar es Salaam, Kigoma, Pwani na kwingineko, imeshuhuudia kufanyika pia mandamano ya kumbukumbu ya Ashura ambapo waandamanaji wameonyesha huba na mapenzi yao makubwa kwa Imamu Hussein (AS) na Ahlul-Bayt (AS).

Nchini Uganda pia Waislamu wa medhehebu ya Shia na wapenzi wa Imam Hussein (AS) huko Uganda wamefanya matembezi ya amani mashariki mwa nchi hiyo, kwa mnasaba wa maombolezo ya Ashura ya Bwana huyo wa Mashahidi.

Huku wakiwa wamevalia mavazi meusi, Waislamu hao wamefanya matembezi ya amani huku wakijipiga vifua, kwa mnasaba wa kumbukumbu ya tukio chungu la kuuawa shahidi Imam Hussein AS katika jangwa la Karbala mwaka 61 Hijria.

Baadhi ya mabango yaliyokuwa yamebebwa na waombolezaji hao yalikuwa na ujumbe usemao "Labbaika Yaa Hussein" huku mengine yakiwa na maandishi yasemayo: Matukio chungu ya Muharram.

Washiriki wengine wa marasimu hayo ya Ashura ya Imam Hussein AS nchini Uganda wameonekana wakimuomboleza mjukuu huyo wa Mtume Muhammad SAW na masahaba zake waaminifu kwa kusoma kasida za maombolezo na kujipiga vifua.

Ijumaa au Jumamosi zimesadifiana na siku ya kumi ya mwezi wa Muharram 1445 Hijria ni siku ya Ashura ya Imamu Hussein AS.  Aba Abdillah Al-Hussein AS na masahaba zake waaminifu waliuawa shahidi huko Karbala mnamo tarehe 10 Muharram mwaka 61 Hijria.

4157253

captcha