IQNA

Jinai za Israel

WHO yataka wakimbizi Wapalestina wafadhiliwe kimataifa

12:14 - January 30, 2024
Habari ID: 3478278
Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya la Umoja wa Mataifa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema katika chapisho la ukurasa wake wa mtandao wa kijamii wa X jana Jumapili kwamba kukata ufadhili kwa UNRWA "kutawaumiza tu watu wa Gaza".

Ameongeza kuwa watu wa Gaza wanakabiliwa na tishio kubwa linalonyemelea la njaa, magonjwa na kufurushwa makwao baada ya karibu miezi minne ya mashambulizi ya mauaji ya kimbari ya utawala haramu wa Israel.

Ombi hilo limekuja baada ya  baadhi ya nchi za Magharibi kusitisha misaada ya kifedha kwa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Wakimbizi la Palestina UNRWA.

Mkuu wa UNRWA, Philippe Lazzarini aliandika katika chapisho kwenye X, zamani Twitter siku ya Jumapili kwamba misaada ambayo UNRWA huwapa wakimbizi Wapalestina inakaribia kumalizika.

Aliendelea kuandika kuwa: "Operesheni yetu ya kibinadamu, ambayo watu milioni 2 wanategemea kama njia ya kuokoa maisha huko Gaza, inasambaratika. Ninashangaa maamuzi kama haya yanachukuliwa kwa mujibu wa mwennendo wa watu wachache  wakati vita vinaendelea, mahitaji yanazidi kuongezeka na njaa inanyemelea." Halikadhalika amesema "Wapalestina wa Gaza hawakuhitaji adhabu hii ya ziada ya pamoja. Hii inatutia doa sote.”

UNRWA imetangaza kwamba inaanzisha uchunguzi baada ya utawala wa Kizayuni wa Israel kudai kuwa baadhi ya wafanyakazi wa shirika hilo walihusika katika operesheni ya tarehe 7 Oktoba ya Kimbunga cha Al-Aqsa dhidi ya utawala huo ghasibu.

Tuhuma hizo zilizotolewa na utawala wa Kizayuni zimesababisha nchi zisizopungua 10 za Magharibi kujiondoa au kusitisha kwa muda misaada yao ya kifedha kwa shirika hilo la UN, hatua ambayo mkuu wa UNRWA amesema ni "ya kushtusha".

Mkuu wa UNRWA ameonya kwamba “Zaidi ya watu milioni mbili huko Gaza wanategemea shirika hilo la Umoja wa Mataifa kwa ajili ya kuishi lakini operesheni yake ya kibinadamu inaporomoka.”

UNRWA ina wafanyakazi 13,000 wanaohudumia jamii za Wapalestina huko Gaza. Leo takriban 3,000 wanaendelea kufanya kazi katika eneo la vita, lililopewa jukumu la kuendesha makazi kwa zaidi ya watu milioni moja, kutoa chakula na huduma za afya kwa raia walio na uhitaji mkubwa tangu kuanza kwa vita.

Hadi sasa, zaidi ya Wapalestina  26,420 wameuawa huko Gaza tangu Oktoba 7 wakati utawala haramu wa Israeli ulipoanzisha vita vya mauaji ya kimbari dhidi ya eneo hilo. Aghalabu ya waliouawa na kujeruhiwa ni wanawake na watoto.

4196712

Habari zinazohusiana
captcha