IQNA

Jinai za Israel

UN: Idadi ya raia waliouawa na utawala wa Israel huko Gaza haina kifani

21:24 - February 16, 2024
Habari ID: 3478363
IQNA-Mkuu wa Kitengo cha Asia Magharibi katika Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa amesema: Idadi ya raia na waandishi wa habari waliouawa huko Gaza haina mfano.

Mohammed Al-Nasour, amelaani jinai za Israel na kuutaka utawala huo wa Kizayuni utoe maelezo kuhusu jinai hizo kubwa za mauaji ulizofanya lakini utawala huo haujatoa jibu lolote juu ya suala hilo.

Kwa mujibu wa tangazo la Mkuu wa Kitengo cha Asia Magharibi katika Ofisi ya Kamishna Mkuu wa Haki za Binadamu wa Umoja wa Mataifa tokea Oktoba 7, 2023 hadi sasa, utawala huo haramu umeshawauawa shahidi wanahabari 110.

Al Nasour amesisitiza kuwa  nchi zenye ushawishi kwa Tel Aviv zinapaswa kuushinikiza zaidi  utawala huo.

Kwa upande mwingine, na katika msimamo wa karibuni zaidi aliotoa kuhusu Gaza, Mufti wa Oman, Sheikh Ahmed bin Hamad al-Khalili, amesisitiza juu ya kuwaunga mkono wakazi wanaodhulumiwa wa eneo hilo.

Huku akiashiria mashambulizi yasiyokoma ya utawala wa Kizayuni dhidi ya mji ya Rafah ambayo yamesababisha mamia ya Wapalestina kuuawa shahidi na kujeruhiwa, Sheikh Al Khalili amesema, "tunashangazwa na kimya cha nchi majirani kuhusiana na jinai hizi; kwamba kwa nini hazichukui hatua yoyote kuwasaidia wanaodhulumiwa?"

Kabla ya hapo, Mufti wa Oman alieleza kuwa hali ya Palestina inayokaliwa kwa mabavu imezidi kuwa mbaya na dhulma imefikia kiwango cha kutisha na akaongezea kwa kusema, watu wanaopambama na wanaodhulumiwa wa Palestina wanataabika kwa njaa, lakini ndugu zao wanawasaliti kwa kumsaidia adui na kumfungulia njia ya kupitishia bidhaa zake.

Mji wa Rafah unahifadhi zaidi ya wakimbizi milioni moja na laki nne wa Kipalestina, na Benjamin Netanyahu, Waziri Mkuu wa utawala wa Kizayuni mteketezaji wa roho za watoto, hivi karibuni alitangaza kuwa mashambulizi makubwa dhidi ya mji huo yataanza kufanywa katika siku zijazo; mashambulizi ambayo yana baraka kamili za rais Joe Biden wa Marekani.

Wakati huohuo imeripotiwa kuwa, idadi kadhaa ya askari wa brigedi ya Gafaati ya jeshi la Kizayuni hivi karibuni walikataa kushiriki katika vita vya Gaza. Askari hao wa Kizayuni walisisitiza kuwa makamanda wao hawajali hali zao za kiafya za kiakili na kimwili. 

Hivi karibuni gazeti la Kizayuni la Ma'ariv lilitoa ripoti na kutangaza  kuwa makumi ya askari wa Kizayuni walioshiriki katika vita vya Ukanda wa Gaza wamepatwa na maradhi mbalimbali na baadhi yao wamechukua hatua ya kujiua.

Kitambo nyuma mtandao wa Kizayuni wa Kan ulikiri katika ripoti uliyotoa kuhusiana na suala hilo kwamba zaidi ya wanajeshi elfu mbili waliopigana vita vya nchi kavu dhidi ya Ukanda wa Gaza wamelazimika kwenda kwa wataalamu wa saikolojia kutokana na kusumbuliwa na matatizo ya akili.

Wakati huohuo, Antonio Tajani, Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia naye pia ameukosoa utawala wa Kizayuni kwa jinai unazofanya huko Gaza na akasema: Wapalestina wengi wamepoteza maisha katika hujuma ya kinyama ya jeshi la Israel katika eneo hilo.

Rais Miguel Diaz-Canel wa Cuba yeye amehutubia kikao katika mji mkuu wa nchi hiyo Havana huku akiwa amevalia skafu ya nembo ya Palestina, ambapo mbali na kulaani uvamizi wa utawala ghasibu wa Kizayuni katika Ukanda wa Gaza amezielezea jinai za Israel kuwa ni za kinyama na mauaji ya kimbari.

Katika upande mwingine, shirika la Madaktari wasio na mipaka  MSF limetoa taarifa na kueleza kuwa hali ya Hospitali ya Nasser huko Khan Yunis ni ya kuhuzunisha na kutia wasiwasi.

Katika taarifa yake hiyo, MSF imewataka wanajeshi katili wa Kizayuni wadhamini usalama wa kada nzima ya tiba, wagonjwa na wakimbizi waliomo hospitalini humo.

Jana asubuhi na kupitia vipaza sauti, wanajeshi wa kizayuni waliwataka watu wote waliopewa hifadhi ndani ya Hospitali ya Nasser waondoke hospitalini humo. 

Waliokuwemo hospitalini humo waliondoka kwa makundi huku wakiwa na wasiwasi mkubwa kuhusu usalama wao, kwa sababu walisikia walikuwa wameshasikia kwamba raia wenzao kadhaa walishambuliwa kwa risasi na askari wa Kizayuni wakati walipokuwa wakitoka hospitalini humo.

Kwa zaidi ya siku 21 sasa, jengo la hospitali ya Nasser limezingirwa jeshi la utawala wa Kizayuni na maji na umeme katika hospitali hiyo vimekatwa.

Wizara ya Afya ya Palestina imetangaza kuwa, idadi ya Wapalestina waliouawa shahidi tangu yalipoanza mashambulio ya mauaji ya kimbari ya utawala wa Kizayuni huko Gaza mnamo Oktoba 7, imepindukia 28,576 na idadi ya waliojeruhiwa ni zaidi ya 68,291.

4200127

Habari zinazohusiana
captcha