IQNA

Taliban yalenga Msikiti Pakistan na kuua watu 24

20:59 - March 31, 2017
Habari ID: 3470914
TEHRAN (IQNA)-Magaidi wakufurishaji wa Taliban wamekiri kutekeleza hujuma iliyolenga msikiti nchini Pakistan na kuua watu 24 na wengine zaidi ya 90 kujeruhiwa.

Maafisa wa usalama wanasema gari lililokuwa limesheni mabomu liliripuka Ijumaa mchana karibu na msikiti mmoja wa mji wa Parachinar kaskazini mashariki mwa Pakistan.

Mushtaq Ghani, msemaji wa serikali ya mkoa, amesema mlipuko huo ulijiri karibu na msikiti ambao wengi wanaoswali hapo ni Waislamu wa madhehebu ya Shia. Msikiti huo uko karibu na Soko la Noor na wengi waliofariki walikuwa wanajitayarisha kushiriki katika sala ya Ijumaa.

Kundi la kigaidi linalojiita Jamaat-ul-Ahrar, ambalo ni tawi la kundi la kigaidi la Taliban nchini Pakistan, kupitia msemaji wake Asad Mansoor, limetangaza kutekeleza hujuma hiyo iliyowalenga Waislamu.

Waziri Mkuu wa Pakistan Nawaz Sharif amelaani hujuma hiyo ya kigaidi na kusema serikali yake inajitahidi kuangamiza ugaidi kikamilifu nchini humo. Hatahivyo viongozi wa Kiislamu eneo hilo wameilaumu serikali kwa kushindwa kuchukua hatua za kuwalinda Waislamu wa madhehebu ya Shia ambao wanakabiliwa na hujuma za mara kwa mara za magaidi wakufurishaji wa pote la Uwahhabi.

Parachinar ni mji mdogo ulio katika eneo la kikabila la Kurram ambalo liko katika mpaka wa Pakistan na Afghanistan na limekuwa likikumbwa na hujuma za kigaidi mara kadhaa. Eneo hilo liliwahi kuwa kitovu cha kundi la kigaidi la Taliban.

3586182

captcha