IQNA

Mgogoro waendelea Marekani baada ya Trump kupinga ushindi wa Biden akidai wizi wa kura

14:33 - November 08, 2020
Habari ID: 3473340
TEHRAN (IQNA)- Vyombo vya habari vya Marekani vimetangaza kuwa mgombea urais kwa tiketi ya chama cha cha upinzani cha Democratic, Joe Biden ndiye aliyechaguliwa na Wamarekani kuwa rais wa 46 wa nchi hiyo lakini Rais Donald Trump anasisitiza yeye ndiye mshindi na kwamba kumekuwepo wizi wa kura.

Ripoti zinasema kuwa Biden ameshinda kura 290 za wajumbe wa Electoral College baada ya kumpiku mpinzani wake, Donald Trump katika majimbo ya Pennsylvania na Nevada. Biden alihitajia kura 270 tu ya kati ya 538 za wajumbe wa Electoral College ili atangazwe mshindi. 

Timu ya kampeni za uchaguzi ya Donald Trump imesema bado ni mapema kumtangaza Joe Biden kuwa mshindi wa uchaguzi wa rais wa tarehe 3 Novemba na kusisitiza kuwa, itawasilisha mashtaka mahakamani dhidi ya jinsi zoezi la uchaguzi wa rais wa Marekani lilivyofanyika. Hata hivyo, kwa kutilia maanani ufa na tofauti kubwa iliyopo baina ya kura za wananchi na zile za wajumbe wa Electoral College za washindani hao wawili ni vigumu sana kuona matokeo yaliyotangazwa na vyombo vikuu vya habari vya Marekani yakibadilika kwa maslahi ya Donald Trump. Hivyo, tunaweza kusema kuwa, Biden ndiye atakayeshika hatamu za uongozi wa Marekani tarehe 20 Januari mwakani baada ya kipindi cha Donald Trump kumalizika rasmi. 

Joe Biden atashika hatamu za uongozi wa nchi inayosumbuliwa na matatizo mengi likiwemo janga la maambukizi ya coona, machafuko ya ubaguzi wa rangi na mpasuko mkubwa wa kisiasa na kijamii. 

Wafuasi wa Trump huku wakiwa wamejizatiti kwa silaha za moto wamemiminika katika barabara na mitaa ya majimbo ya Arizona na Georgia, kulalamikia ushindi wa Joe Biden katika uchaguzi wa rais wa nchi hiyo.

3933804

Kishikizo: biden trump marekani
captcha