IQNA

Wanawake Waislamu katika Jeshi la Afrika Kusini wapata idhini kuvaa Hijabu

16:36 - January 29, 2021
Habari ID: 3473600
TEHRAN (IQNA) - Jeshi la Afrika Kusini limefanyia marekebisho kanuni zake za uvaaji na sasa limewaruhusu askari wanawake wa Kiislamu nchini humo kuvalia vazi la stara la hijabu wakiwa kazini.

Mafi Mgobozi, Msemaji wa Jeshi la Ulinzi la Afrika Kusini (SANDF) amethibitisha habari hizo za kufutwa marufuku ya kuvaa hijabu kazini kwa wanawake wa Kiislamu wanaohudumu jeshini nchini humo.

Uamuzi huo ni ushindi mkubwa kwa wanajeshi wa kike wa Kiislamu nchini humo, ambao kwa miaka mingi hawakuwa wanaruhusiwa kuvaa vazi hilo la staha.

Meja Fatima Isaacs, afisa wa ngazi ya juu wa jeshi la Afrika Kusini kwa muda wa miaka mitatu amekuwa katika mpambano wa kisheria wa kutaka askari jeshi wa Kiislamu nchini humo waruhusiwe kuvalia hijabu wakiwa kazini.

Januari mwaka jana, Mahakama ya Kijeshi nchini humo ilimuondolewa shitaka Meja Fatima, la kuvaa hijabu chini ya kofia yake ya kijeshi akiwa kazini.

Baada ya uamuzi huo, Meja Fatima Isaacs ambaye ni mwanapatholojia katika Hospitali ya Kijeshi nchini humo ameliambia gazeti la Cape Times kuwa, "huu si ushindi kwangu mimi tu, bali kwa watu wote ambao wanabinywa na kunyimwa haki zao kimya kimya."

Amesema Afrika Kusini ni nchi ya kidemokrasia na inapaswa kuheshimu mafundisho na haki za watu wa dini zote.

3950435

captcha