IQNA

Qur'ani Inasema nini / 6

Ahadi ya Mwenyezi Mungu ya Kumjibu Mwombaji

13:09 - June 12, 2022
Habari ID: 3475367
TEHRAN (IQNA) – Mwanadamu humwita Mwenyezi Mungu anapokabiliwa na matatizo na kuomba msaada lakini wakati fulani inaonekana kwamba hakuna jibu. Je, hii inamaanisha kwamba mtu anapaswa kufikiria upya kumwomba Mwenyezi Mungu msaada?

Kwa kila mwanadamu, kunaweza kuwa na nyakati maishani ambapo hajui jinsi ya kuzungumza na Mwenyezi Mungu.

Baadhi ya Waislamu walikwenda kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) wakimuuliza kuhusu hili. Walitaka kujua jinsi ya kumwita Mwenyezi Mungu.

Kisha ikateremshwa aya ya 186 ya Surah Al-Baharah ya Qur'ani Tukufu isemayo:

"Na waja wangu watakapo kuuliza khabari zangu, waambie kuwa Mimi nipo karibu. Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba. Basi na waniitikie Mimi, na waniamini Mimi, ili wapate kuongoka."

 

Kumuomba Mwenyezi Mungu kunamaanisha kuzungumza naye na kumhisi yuko karibu. Maombi ni uhusiano na Mwenyezi Mungu moyoni. Kumwomba Mwenyezi Mungu huonyesha mtu ana matumaini atapa jibu. Ikiwa hatungekuwa na tumaini lolote kwamba maombi yetu yatajibiwa, hatungetaka chochote kutoka kwa Mungu.

Katika Tafsiri yake ya Nur ya Quran Tukufu, Khatibu Hujjatul Islam Sheikh Muhsim Qara’ati anasema hivi kuhusu aya hii:

Kuomba au Dua ni muhimu wakati wowote na popote inapofanyika kwa sababu Mwenyezi Mungu anasema: "Mimi nipo karibu" na kuwa kwake karibu ni milele. Lakini vipi sisi? Je, tuko karibu Naye daima? Iwapo wakati fulani anatukasirikia, ni kwa sababu tunajiweka mbali Naye kutokana na dhambi zetu.

Kujibu maombi ni hakika na hufanyika kila wakati. Maombi au Dua hujibiwa wakati yanapoambatana na imani, kama Mungu asemavyo, " na waniamini Mimi ".

Jambo lingine ni kwamba maombi ni njia ya ukuaji na mwongozo: “… ili wapate kuongoka.”

Swali ni kwa nini baadhi ya maombi hayajibiwi ingawa Mwenyezi Mungu anasema: “Naitikia maombi ya mwombaji anapo niomba”?

Kwa mujibu wa Sheikh Qara’ati, baadhi ya sababu ni kama zifuatazo:

- Baadhi ya matendo kama vile kutenda madhambi, kuwadhulumu wengine, na kupata pesa au rizki ya Haramu kunaweza kuzuia kuitikiwa kwa maombi.

- Wakati fulani dua ya mtu haijibiwi lakini kitu sawa au kinachoshabihiana na kile alichokiomba.

- Wakati mwingine matokeo ya dua au maombo huja baadaye au hata majibu hufikia familia au kizazi chake cha baadaye. Aidha wakati fulani ombi halijibiwi mara moja lakini litajibiwa Siku ya Kiyama.

- Maombi yoyote ambayo hayajibiwi kwa hakika sio maombi kwa sababu maombi maana yake ni kuomba mema lakini mambo mengi tunayoomba yanaweza yasiwe mazuri.

Habari zinazohusiana
captcha