IQNA

Qur'ani Tukufu Inasemaje/17

Jinsi ya kuzuia kuporomoka jamii

18:45 - July 12, 2022
Habari ID: 3475495
TEHRAN (IQNA) – Qur’ani Tukufu inadhihirisha kwamba matendo ya watu binafsi yana athari kubwa na ya moja kwa moja kwa jamii kwani haitoshi kutegemea sheria kali za kijamii kwa ajili ya kurekebisha jamii; badala yake, kuwe na juhudi za kukuza uelewa miongoni mwa wanajamii.

“Amali njema” na “ufisadi” ni dhana mbili kinyume na kwa mujibu wa mafundisho ya Kiislamu athari ya amali njema inaweza kudhihirika kwa wenye haki na wake weme huku ile ya ufisadi ikidhihirika wazi miongoni mwa wapotovu.

Lakini nini maana ya dhambi na ufisadi na nini tofauti yao?

Dhambi ni kitendo cha mtu binafsi ambacho kinachukuliwa kuwa ni kutotii amri za Mwenyezi Mungu, kwa maneno mengine, maana yake ni kufanya jambo ambalo Mwenyezi Mungu amekataza au kuacha jambo ambalo Ameamuru kulifanya. Na ufisadi ni hali inayovuruga njia ya kawaida ya jamii, kuharibu uhuru, usalama, haki, na amani ya umma na kuvuruga usawa wa jamii.

Kwa hiyo, dhambi ni matokeo ya matendo ya watu binafsi wakati ufisadi unahusiana na jamii; Qur'ani imeweka wazi  uhusiano wa moja kwa moja kati ya nukta hizo mbili. “Ufisadi umedhihiri bara na baharini kwa iliyo yafanya mikono ya watu, ili Mwenyezi Mungu awaonyeshe baadhi ya waliyo yatenda. Huenda wakarejea kwa kutubu..” (Surah Ar-Rum, aya ya 41)

Aya hii inaonyesha uhusiano mkubwa kati ya dhambi na ufisadi. Dhambi ni kama chakula kisicho na afya ambacho kina athari mbaya kwa mwili, na kusababisha mfululizo wa athari ambazo ni lazime ziibuke. Kwa mfano, uwongo huondoa uaminifu, usaliti hupotosha mahusiano ya kijamii, na sikuzote uonevu au dhulma huibua dhulma au uonevu mwingine.

Kwa mujibu wa riwaya za Kiislamu, madhambi mengi yana madhara ambayo yamefichika kwetu. Kwa mfano, imetajwa katika riwaya kwamba kukata mahusiano na familia kutafanya maisha kuwa mafupi na kuchukua mali ya yatima kutafanya moyo kuwa ni wenye giza.

Mtume Muhammad (SAW) amenukuliwa akisema katika Hadith kwamba “Baada yangu, itakapodhihirika waziwazi zinaa miongoni mwa watu, vifo visivyotarajiwa vitaongezeka; watakapofanya ulaghai (kuhusu kupima na wizani), Mwenyezi Mungu atawaletea ukame; watakapojizuia kutoa Zaka, watasaidiana wao kwa wao katika kuzidisha dhulma na uadui; watakapovunja mapatano, Mwenyezi Mungu atawaleta maadui miongoni mwao; na watakapoacha kuamrisha mema na kukataza maovu na wasiwafuate Ahlul-Bayt wangu, watajaaliwa kuwa na watawala  wabaya.”

Ni Sunna ya Mwenyezi Mungu kwamba ikiwa watu hawatajihusisha katika kujirekebisha, kwa kawaida ulimwengu utafanya hivyo kwa sheria za Kkimungu, kuondoa makosa. Mfasiri maarufu wa Qur'ani aliyeandika Tafsir Al Mizan, Allamah Tabatabai, anaitaja Quran na kubainisha kwamba ubaya hautadumu duniani na dunia iko kwenye njia ya kuboreka. “...Hakika Mwenyezi Mungu hawaongoi watu wenye kudhulumu.” (Surah Al-Ma'idah, aya ya 51)

Habari zinazohusiana
captcha