IQNA

Mgogoro wa Iraq

Iran yatumai mgogoro wa Iraq utatatuliwa kwa mazungumzo

12:43 - August 30, 2022
Habari ID: 3475702
TEHRAN (IQNA)- Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran amesisitiza haja ya kuhifadhiwa umoja wa kitaifa wa Iraq, akisema matatizo ya nchi hiyo yanapaswa kutatuliwa kwa njia za kisheria.

Hossein Amir-Abdollahian aliyasema hayo katika mkutano wa Jumatatu na mwenzake wa Iraq, Fuad Hossein, mjini Tehran.

Katika mkutano huo mwanadiplomasia mkuu wa Iran ameashiria ulazima wa kulindwa utulivu, amani na umoja wa kitaifa nchini Iraq, akitoa wito kwa makundi yote ya kisiasa kuheshimu taasisi za kisheria za nchi hiyo ya Kiarabu.

Pia alitoa wito wa kupanuliwa zaidi kwa ushirikiano wa kibiashara na kiuchumi kati ya Iran na Iraq kwa kutumia fursa zao zilizopo.

Waziri wa Mambo ya Nje wa Iraq kwa upande wake amesema usalama wa Iran na Iraq umefungamana na kusisitiza kuwa nchi yake haitaruhusu eneo lake kutumika kwa ajili ya kuleta tishio lolote kwa Jamhuri ya Kiislamu.

Iraq imekuwa katika mkwamo wa kisiasa tangu uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka jana. Vyama hasimu vimeshindwa kuafikiana kuhusu kuundwa kwa serikali mpya, hivyo kusababisha maandamano na hujuma ya wafuasi wa makundi ya kisiasa dhidi ya bunge.

Muungano wa kisiasa unaoongozwa na msomi mashuhuri wa Kiislamu Muqtada al-Sadr uliibuka kama mrengo mkubwa zaidi wa wabunge katika uchaguzi huo, lakini ukakosa kupata wingi kamili uliohitajika kuunda serikali, na kusababisha mkwamo wa kisiasa uliopo nchini humo.

Mnamo Juni, wabunge wote 73 wa kambi hiyo ya Sadr walijiondoa katika viti vyao katika hatua inayoonekana kama jaribio la kuwashinikiza wapinzani wa kisiasa kuharakisha kuundwa kwa serikali.

Muqtada al-Sadr na wafuasi wake wamesaidia kuzusha hali ya wasiwasi katika muda wa wiki mbili zilizopita huku maelfu ya wafuasi wake wakivamia na kulikalia bunge la nchi hiyo na kuzuia kuundwa kwa serikali karibu miezi 10 baada ya uchaguzi uliopita.

Mapema Jumatatu, Muqtada al-Sadr  alitangaza kwamba anajiondoa rasmi katika kisiasa na kufunga ofisi zake za kisiasa.

Katika taarifa yake, Sadr pia aliwashambulia wapinzani wake wa kisiasa, akisema kuwa wameshindwa kutii wito wake wa kutaka mageuzi.

Kufuatia tangazo hilo, wafuasi wa Sadr walivamia Ikulu ya Republican, ambayo ni jengo la sherehe rasmi ndani ya Ukanda wa Kijani wenye ulinzi mkali mjini Baghdad  ambapo wamepambana na vikosi vya usalama.

Jumatatu jioni, Kamandi ya Operesheni ya Pamoja ya Iraq iliweka amri ya kutotoka nje katika mikoa yote nchini humo. Kwa mujibu wa madaktari wa Iraq na vyanzo vya polisi, hadi sasa watu 12 wameuawa na wengine 270 wamejeruhiwa katika mapigano katika mji mkuu Baghdad.

4081805

captcha