IQNA

Mawaida

Muhtasari kuhusu Siku ya Mubahala

15:23 - July 12, 2023
Habari ID: 3477269
Tarehe 24 Dhul-Hijjah husadifiana ni siku muhimu ya katika historia ya Uislamu, ambayo ni maarufu kama Siku ya Mubahalah .

Siku hii ni muhimu sana kutokana na ukweli kwamba katika siku hii, Mtume wa Uislamu (saw) na kwa amri ya Mwenyezi Mungu alikaribia kulaaniana na Wakristo wa Najran katika Bara Arabu kutokana na ukaidi wao wa kutotaka kukubali ukweli. Hili ni moja ya matukio makubwa yaliyosajiliwa katika historia ya mwanzo wa Uislamu, na ambalo linathibitisha usahihi wa wito na ujumbe wa Mtume Mtukufu (saw) na fadhila za watukufu alioandamana nao siku hiyo, ambao si wengine bali ni Imam Ali, Bibi Fatima na Maimam Hassan na Hussein (as).

Tukio la Mubahalah lilitokea tarehe 24 Dhul-Hijjah mwaka wa tisa Hijria, na Aya ya 61 ya Suratul Imran inajulikana kama Aya ya Mubahalah kutokana na umuhimu wake wa kihistoria.

Tukio hilo limetajwa sehemu nyingi katika vitabu na vyanzo vya madhehebu zote mbili za Kiislamu yaani Shia na Sunni. Mashia wanaamini kwamba kwa mujibu wa Aya hiyo ya kitabu kitakatifu cha Qur'ani, nafsi ya Imam Ali (as) ni sawa na nafsi ya Mtume Mtukufu (saw).

Kwa mujibu wa vyanzo vya Kiislamu na kihistoria, baada ya kujadiliana na Wakristo wa Najran ambao mwishowe hawakumwamini, Mtume  (saw) alitoa pendekezo la kufanyika Mubahalah yaani kuomba dua kwa unyenyekevu na kutaka laana ya Mwenyezi Mungu iwateremkie wanaosema uongo, ambapo awali Wakristo hao walikubaliana na pendekezo hilo. Lakini siku hiyo ilipowadia, Wakristo wa Najran walikataa kufanya Mubahalah na Mtume baada ya kuona nyuso takatifu na tukufu za watu aliokuwa ameandamana nao.

Kama tulivyotangulia kusema, Mubahalah ni maombi ya laana ya Mwenyezi Mungu kwa ajili ya kuthibitisha usahihi wa jambo baina ya pande mbili ambazo kila moja inadai kuwa upande wa haki.

3484316

Kishikizo: mubahala
captcha