IQNA

Al Azhar yataka hatua za kimataifa zichukuliwe kukabiliana na chuki dhidi ya Uislamu

18:48 - November 04, 2020
Habari ID: 3473327
TEHRAN (IQNA)- Sheikh Mkuu wa al Azhar nchini Misri amekosoa matamshi ya chuki na hujuma ya Rais Emmanuel Macron wa Ufaransa dhidi ya Uislamu na kutoa wito wa kutungwa sheria inayotambua chuki na uhasama dhidi ya Waislamu kuwa ni uhalifu.

Sheikh Ahmed El-Tayeb ameitaka jamii ya kimataifa kubuni sheria ambayo itatambua uhasama dhidi ya Waislamu na kuenenza chuki baina ya Waislamu na wafuasi wa dini nyingine kuwa ni uhalifu na jinai, na wahusika waadhibiwe.

Sheikh wa al Azhar ameashiria mauaji ya mwalimu Samuel Paty aliyekuwa akiwaonyesha wanafunzi wake darasani vibonzo vinavyomdhalilisha Mtume Muhammad (saw) huko Ufaransa na kusema: Al Azhar ililaani papo hapo kitendo hicho lakini inatambua kuwa kitendo cha kusambaza vibonzo hivyo kina sababisha madhara na ni uhasama wa waziwazi dhidi ya dini ya Uislamu na Mtume wa Mwenyezi Mungu, Muhammad SAW.

Sheikh wa al Azhar pia amewahimiza Waislamu kushikamana na njia za amani na utawala wa sheria kwa ajili ya kulinda na kutetea dini yao na Mtume Muhammad (saw). 

Baada ya mauaji ya mwalimu huyo wa Kifaransa, Rais Emmanuel Macron alitoa matamshi ya jeuri dhidi ya Uislamu na kutangaza kuwa, Ufaransa utaendelea kusambaza katuni na vibonzo vinavyomdhalilisha Mtume Muhammad (saw).

Matamshi hayo ya Macron yamekosolewa sana na Waislamu katika uga wa kimataifa.

3473025

 

captcha