IQNA

Waislamu Ujerumani

Adhana ya kwanza kwa vipaza sauti katika Msikiti wa Jamia ya Cologne, Ujerumani

15:00 - October 15, 2022
Habari ID: 3475931
TEHRAN (IQNA)- Kwa mara ya kwanza kabisa, Adhana imesikika katika moja kati ya misikiti mikubwa zaidi nchini Ujerumani mjini Cologne.

Idhini ya adhana imetolewa lakini kwa sauti ya chini kwa mujibu wa kanuni zilizowekwa na wakuu wa mji huo na ni sehemu ya mapatano mapatano baina mji wa Cologne ambao una moja kati ya jamii kubwa zaidi za Waislamu barani Ulaya.

Wakuu wa mji huo ambao ni wa nne kwa ukubwa Ujerumani wameruhusu misikiti iombe idhini ya kutumia vipaza sauti wakati wa adhana kwa muda wa dakika tano kati ya saa sita na saa tisa mchana siku za Ijumaa. Kiwango cha sauti kitaainishwa kwa mujibu wa eneo ulipo msikiti.

Hii si mara ya kwanza adhana kuruhusiwa misikitini Ujerumani lakini  idhini hiyo mjini Cologne imetangazwa kuwa ya kipekee kutokana na umuhimu wa msikiti huo.

Msikiti wa Jamia wa Cologne ni wa kisasa na una minara miwili mikubwa huku ukiwa katika mtaa wa Ehrenfeld wenye msongamano mkubwa. Msikiti huo wneye uwezo wa kubeba waumini 1,200 ulifunguliwa rasmi na Rais Recep Tayyip Erdogan wa Uturuku mwaka 2018 na unasimamiwa na Jumuiya ya Kiislamu ya Uturuki (DITIB). Hadi sasa adhana ilikuwa inaruhusiwa tu ndani ya msikiti bila vipaza sauti vya nje.

Idhini hiyo ya adhana imetolewa kwa muda wa majaribio wa miaka miwili ambapo  sauti haipasi kupita desibeli 60.

Katibu Mkuu wa DITIB Abdurrahman Atasoy amesema wanafuraha kwani adhana kusikaka nje ya msikiti ni ishara kuwa mji huo ni makao ya Waislamu. Meya wa Cologne amesema kuruhusu adhana kunaoneysha kuwa wakuu wa mji wanathamini uwepo watu wa jamii na dini mbali mbali.

Kuna Waislamu zaidi ya milioni tano nchini Ujerumani na idadi hiyo ni takribani asiimia sita ya watu wote wa nchi hiyo. Mji wa Cologne pekee una wakazi 100,000 Waislamu.

3480844

captcha