IQNA

Chuki dhidi ya Uislamu

Ushindi wa mrengo wa kulia wenye misimamo mikali katika uchaguzi wa Uholanzi na wasiwasi wa Waislamu

21:06 - November 25, 2023
Habari ID: 3477945
UHOLANZI (IQNA)- Uchaguzi mkuu wa Uholanzi ulifanyika Jumatano, Novemba 22 nchini humo ili kubaini nani ataongoza serikali ijayo ambayo inapaswa kuchukua mamlaka nchini baada ya kuondoka Mark Rutte, ambaye amekuwa waziri mkuu kwa miaka 13.

Matokeo ya uchaguzi wa bunge la Uholanzi yanaonyesha kuwa chama chenye misimamo mikali cha "Party for Freedom" kinachoongozwa na Geert Wilders kimeshinda uchaguzi huo. Chama hicho kimevishinda vyama vingine hasimu kwa kupata viti 35. Muungano wa Kushoto umeshinda viti 26 na chama cha "People for Freedom and Democracy" kikapata viti 23.

Hata hivyo, chama cha "For Freedom" hakikuweza kushinda wingi mutlaki wa viti. Iwapo matokeo ya kuhesabu kura yataendelea kwa njia hiyo hiyo na Geert Wilders mwenye misimamo mikali ya kupindukia mipaka wa mrengo wa kulia kupata wingi wa viti, itamlazimu aunde muungano na vyama vingine ili kubuni serikali. Katika hali hiyo, mtu huyo mwenye misimamo ya kufurutu ada itachukua nafasi ya Mark Rutte, waziri mkuu wa sasa wa Uholanzi.

Wapinzani wa Uislamu

Geert Wilders alisema Jumatano usiku kwamba: "Waholanzi wanatumai kwamba wataweza kurudisha nchi yao mikononi na tutahakikisha kuwa tsunami ya wahamiaji na wanaotafuta hifadhi itapungua." Huku akitoa wito kwa vyama vingine kushirikiana kwa ajili ya kuunda serikali ya mseto, amesema chama chake hakiwezi "kupuuzwa" tena. Chama cha "For Freedom" ni miongoni mwa vyama vya siasa kali za mrengo wa kulia vinavyopinga wahajiri na Uislamu nchini Uholanzi, na ushindi wake unaweza kuwa na taathira kubwa katika uhusiano wa nchi hiyo na Umoja wa Ulaya. Chama hicho kimeweza kuvutia hisia za Waholanzi kwa kauli mbiu zinazopinga uhamiaji. Suala la uhamiaji limekuwa mojawapo ya masuala muhimu na yenye changamoto kubwa katika kampezi za uchaguzi nchini Uholanzi, jambo ambalo lilimpelekea Mark Rutte, ambaye amekuwa na rekodi ya serikali iliyodumu kwa muda mrefu zaidi katika historia ya nchi hiyo, kutowania tena nafasi hiyo.

Kengele ya Hatari

Ushindi wa wanasiasa hao wa mrengo wa kulia katika uchaguzi wa bunge la Uholanzi kwa mara nyingine tena umepiga kengele ya hatari kwa Umoja wa Ulaya unaopigania kuwepo mshikamano zaidi wa nchi za Ulaya, na hivyo kuongeza uwezekano wa kusambaratika taasisi hiyo ya Ulaya. Chama chenye misimamo ya kufurutu ada cha "For Freedom" kinachoongozwa na Geert Wilders, ambaye hajawahi kuhudumu katika serikali ya Uholanzi, ni moja ya mirengo ya kisiasa ya nchi hiyo, ambao umekuwa ukizingatiwa sana na watu wa Uholanzi, na sasa kufuatia ushindi wake katika uchaguzi wa bunge, unaweza kubuni muungano na vyama vingine na hatimaye kuunda serikali mpya ya nchi hiyo. Serikali ambayo bila shaka itakuwa na mtazamo wa kupinga uhamiaji, sawa kabisa na kama zinavyofanya serikali nyingine za mrengo wa kulia za Ulaya kama vile Poland na Hungary, na hivyo kukabiliana moja kwa moja na maamuzi ya Umoja wa Ulaya, hasa kuhusu suala la wahamiaji. Aidha, Geert Wilders anahesabiwa kuwa miongoni mwa wanasiasa mashuhuri wanaopinga Uislamu barani Ulaya, hivyo ni wazi kwamba atachukua hatua na kuongeza mashinikizo dhidi ya Waislamu wanaoishi Uholanzi katika utawala wake.

Kabla ya hapo, ushindi mpya wa vyama vya mrengo wa kulia nchini Ujerumani na Ugiriki uliangazia tena suala la Ulaya kugeuza mkondo kuelekea siasa kali za mrengo wa kulia, suala ambalo limeibua wasiwasi mkubwa miongoni mwa viongozi wa Ulaya.

Chama cha Mbadala cha Ujerumani cha mrengo mkali wa kulia (AfD) kilishinda uchaguzi wake wa kwanza wa mabaraza ya mitaa mwishoni mwa Juni 2023 baada ya kura za maoni kuonyesha ongezeko la uungaji mkono wake nchini. Kusini mwa Ulaya, huko Ugiriki pia, chama cha mrengo wa kulia cha "Demokrasia Mpya" kinachoongozwa na waziri mkuu wa zamani wa Ugiriki "Kriakos Mitsotakis" kilishinda uchaguzi wa bunge.

Tishio kubwa

Nafasi ya vyama na harakati za mrengo wa kulia zenye misimamo ya kupindukia mipaka inaendelea kuimarika siku baada ya siku katika nyanja za kisiasa za nchi za Ulaya. Kimsingi, kuingia madarakani vyama na viongozi wenye misimamo mikali wa mrengo wa kulia kunachukuliwa kuwa tishio kubwa kwa msikamano wa nchi za Ulaya na Umoja wa Ulaya, kwa sababu vyama hivyo na viongozi wao wanataka kupewa kipaumbele kujitawala na maslahi ya kitaifa kabla ya kuzingatiwa mamlaka na maslahi ya Umoja wa Ulaya. Hivyo kuhusu masuala mengi kama vile ya uhamiaji na wanaotafuta hifadhi katika nchi za Ulaya pamoja na sera za kiuchumi na kijamii, viongozi hao hawako tayari kufuata maamuzi ya Brussels. Aidha, vyama hivyo vina mielekeo ya uzalendo kupindukia na hivyo kutaka kufukuzwa wahamiaji kutoka nchi za Ulaya. Wakati huohuo, vingi vya vyama hivyo vina mielekeo ya chuki dhidi ya Uislamu na Waislamu ambao wanaunda idadi kubwa ya wahamiaji katika nchi hizo.

Ni kutokana na ukweli kwamba vitendo vya unyanyasaji dhidi ya jamii za waliowachache na wahamiaji vinachochewa na vyama vyenye misimamo ya chuki dhidi ya wageni ndio maana viongozi wa Ulaya wakavichukulia kuwa tishio kubwa kwa usalama wa nchi za Ulaya. 

Habari zinazohusiana
captcha