IQNA

Palestina yalaani raia wa UAE waliofika Al Aqsa kwa ulinzi wa jeshi la Israel

16:20 - October 20, 2020
Habari ID: 3473279
TEHRAN (IQNA)- Waziri Mkuu wa Palestina amelaani kitendo cha kuruhusiwa ujumbe wa Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kuingia ndani ya Msikiti wa al Aqsa katika mji wa Quds (Jerusalem) huku Wapalestina wakizuiwa kuswali katika msikiti huo.

Mohammad Shtayyeh amesema kuwa, inasikitisha kuona ujumbe wa baadhi ya nchi za Kiarabu ukiruhusiwa kuingia katika Msikiti wa Aqsa wakati utawala haramu wa Israel ukiwazuia Wapalestina kutekeleza ibada ya Swala katika eneo hilo takatifu na kusema jambo hilo linawaumiza sana Wapalestina.

Waziri Mkuu wa Palestina ameongeza kuwa, kuingia katika eneo hilo takatifu kunapaswa kufanyika kupitia mlango wa Wapalestina ambao ndio wamiliki halisi wa Msikiti wa al Aqsa.

Ni vyema kukumbusha hapa kuwa Jumapili ya jana Wapalestina wanaoishi Quds Tukufu waliutimua ujumbe wa Imarati uliongia katika Msikiti wa al Aqsa chini ya ulinzi wa polisi wa utawala haramu wa Israel.

Ripoti zinasema, Wapalestina waliokuwa na hasira waliwafukuza Waimarati hao wakati walipokuwa wakitembelea eneo Qubbatu Sakhrah na kupiga picha ndani ya msikiti huo mtakatifu na kuwataka waondoke eneo hilo mara moja.

Wapalestina hao walikuwa wakipiga nara zinazopinga hatua ya Imarati ya kuanzisha uhusiano rasmi na utawala haramu wa Israel. 

Tarehe 15 Septemba mwaka huu, Mawaziri wa Mashauri ya Kigeni wa UAE na Bahrain walitia saini makubaliano ya kutangaza uhusiano wa kawaida baina ya nchi zao na utawala ghasibu wa Israel.

3472888

captcha