IQNA

Sura za Qur'ani Tukufu /11

Sura ya Qur'ani Tukufu Iliyomfanya Mtume Mtukufu SAW Kuzeeka

11:23 - June 19, 2022
Habari ID: 3475397
TEHRAN (IQNA) – Pamoja na aya zinazozungumzia rehema ya Mwenyezi Mungu, kuna aya katika Qur’ani Tukufu zinazozungumzia uadilifu wa Mwenyezi Mungu na jinsi wakandamizaji na madhalimu wanavyoadhibiwa. Baadhi ya aya kama hizo zimo katika Surah Hud.

Picha iliyosawiriwa katika Sura ya jinsi watenda maovu wanavyoadhibiwa ni kubwa mno kiasi kwamba Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) amenukuliwa akisema kwamba Sura hii ilimfanya kuzeeka.

Surah Hud ni sura ya 11 ya Qur'ani Tukufu na ina aya 123. Ni Sura ya Makki (ya Makka), yaani, imeteremshwa Makka. Surah Hud imo katika Juzuu za 11 na 12 za Quran na ni Sura ya 52 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume (SAW). Kwa sehemu Fulani inahusiana na Mtume Hud.

Nabii Hud alikuwa Mtume wa Mwenyezi Mungu ambaye aliteuliwa kuwa mtume miaka 700 hivi kabla ya Nabii Issa Masih (AS) katika sehemu za kusini za Arabia. Jina lake limetajwa katika Qur'ani Tukufu mara kadhaa na mojawapo ya Sura za Kitabu kitukufu pia imeitwa kwa jina lake.

Surah Hud iliteremshwa Makka kabla tu ya Hijra ya Mtukufu Mtume (SAW) kwenda Madina. Ilikuwa ni wakati ambao kabla yake,  Mtukufu Mtume (SAW) alikuwa amempoteza ami yake na mke wake. Ndio maana Sura inaanza na sentensi alizoambiwa Mtume (SAW) ili kumfariji. Kisha inapitia magumu ambayo wajumbe wa Mungu waliotangulia walipitia na ushindi walioupata.

Hadithi za manabii kama Nuh, Hud, Saleh, Lut, Ibrahim na Musa, matatizo waliyoyapitia ili kuwaongoza watu na adhabu walizopewa watu kwa matendo yao maovu na dhulma zao zimetajwa katika sura hii ya Qur'ani Tukufu. Kwa mujibu wa Sura hii, siku zote ushindi umekuwa wa Mitume wa Mwenyezi Mungu, ingawa hawakuwa na wasaidizi na masahaba wengi.

Aya nne za kwanza za Sura ni pamoja na mafundisho ya Qur'ani ambayo yamefafanuliwa katika sehemu nyingine ya sura. Mafundisho haya yanahusu Tauhidi, Utume, Ufufuo, na maelezo ya ahadi za Mungu kwa waaminifu na watenda mema.

Kuna aya katika Sura hii kuhusu Siku ya Kiyama au ufufuo, mahakama ya haki ya Mwenyezi Mungu na adhabu zinazotolewa kwa wale waliofanya dhulma katika uhai wao. Ndio maana katika Hadithi ya Mtukufu Mtume (SAW) anasema: “Surah Hud Imenifanya Nizeeke.”

Abdullah ibn Abbas amenukuliwa akisema katika kufasiri Hadithi hii kwamba hakuna Aya nyingine ambayo imekuwa ngumu zaidi kwa Mtume (SAW) kuliko Aya ya 112 ya Surah Hud: “(Muhammad), basi, simama sawa sawa kama ulivyo amrishwa, wewe na wale wanao elekea kwa Mwenyezi Mungu pamoja nawe; wala msikiuke mipaka. Hakika Yeye anayaona yote myatendayo."

Habari zinazohusiana
captcha