IQNA

Sura za Qur’ani Tukufu / 36

Sura Yaseen; Moyo na Kiini cha Qur’an

22:02 - October 27, 2022
Habari ID: 3475996
TEHRAN (IQNA) – Kuna masuala na mada tofauti tofauti zilizotajwa ndani ya Qur’ani Tukufu, huku zile kuu na muhimu zikihusiana na kanuni tatu za dini, yaani Tauhidi, Utume na Ufufuo.

Surah Yaseen au Yasin in ni miongoni mwa sura zinazozungumzia masuala haya makubwa.

Yaseen ni Sura ya 36 ya Qur’ani Tukufu. Ina Aya 83 na iko katika Juzu za 22 na 23. Yasin ni Makki na ilikuwa ni sura ya 43 iliyoteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW).

Inaanza na Huruf al Muqatta'at (herufi zilizotengana) za 'Ya' na 'Seen' na hilo pia likawa chimbuko la sura hii. Kwa mujibu wa Hadith, Yasin ni miongoni mwa Sura zenye hadhi ya juu zaidi katika Qur’ani Tukufu.

Sura Yaseen inajulikana kama "Moyo wa Qur'an" kwani baadhi ya wanachuoni wanaamini kwamba  inajumuisha masomo ya jumla yaliyotajwa ndani ya Qur'an na kwamba ikiwa mtu atazingatia sana sura hii, ni kama ameelewa yote yaliyomo katika  Qur’ani.

Sura Yaseen iliteremshwa kwa Mtukufu Mtume Muhammad (SAW) pale makafiri walipokanusha suala la ufufuo na Mwenyezi Mungu Mtukufu akateremsha Sura hii kuwajibu.

Sura inaelekeza kwenye kanuni tatu za Tauhidi, Utume na Ufufuo. Inazungumzia ufufuo wa wafu na jinsi viungo vitakavyozungumza Siku ya Kiyama.

Aya za kuanzia zinarejea kwenye suala la Utume, falsafa yake na jinsi watu wanavyoitikia mwaliko wa Mitume wa Mwenyezi Mungu. Wanasisitiza kwamba matokeo ya kukubali mwaliko ni uamsho wa watu na kwamba wale wanaokubali wito huu ndio tu watakaokuwa kwenye njia ya wokovu.

Kisha kuna aya kuhusu Tauhidi na dalili za upweke wa Mungu.

Sehemu inayohusu Siku ya Kiyama ndiyo sehemu muhimu zaidi ya Sura. Aya hizi zinahusu ufufuo wa wafu, kutenganishwa kwa wenye kutenda dhambi na wenye kufuata njia ya haki, jinsi watu wanavyoulizwa maswali, mwisho wa dunia,  jehanamu na Janaa..

Aya za kumalizia zinaeleza hali za watenda dhambi na watenda mema siku hiyo kisha kuna mjadala mfupi kuhusu kanuni tatu za Tauhidi, Utume na Ufufuo.

Pia kuna hadithi katika Sura hii kuhusu ujumbe wa watu watatu waliotumwa kwenye mji kuwaalika watu kumwabudu Mwenyezi Mungu. Katika baadhi ya vyanzo, hao watatu wanarejelewa kuwa malaika wa Mwenyezi Mungu au wajumbe wa Yesu (AS).

Watu waliukataa wito wao na mtu mmoja tu ndiye aliyeukubali na akawa muumini. Aliwahimiza wengine kuamini lakini watu wa mji walimuua na kisha wakawa ni wenye kuadhibiwa na Mwenyezi Mungu.

Jina la mtu huyu halikutajwa katika Qur’an, lakini katika Hadithi, amesifiwa na kuitwa Habib Seremala. Inasemekana kwamba alizikwa huko Antakya (Antiokia), ambayo sasa iko nchini Uturuki.

Habari zinazohusiana
captcha